Ujenzi Uwanja wa KMC kugharimu Sh2.7bilioni kwa miezi sita
Muktasari:
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetiliana saini ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Mwenge na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) utakaogharimu Sh2.7 bilioni.
Dar es Salaam.Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetiliana saini ya ujenzi wa Uwanja wa soka wa Mwenge na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) utakaogharimu Sh2.7 bilioni.
Utiliaji saini huo ulifanyika leo Jumatatu Januari 27, 2020 kati ya Meya wa Manispaa Kinondoni, Benjamin Sitta na Mkuu wa Kikosi 361 kampuni wa JWTZ, Luteni Kanali David Luoga hafla iliyofanyika katika ofisi za Manispaa hiyo zilizopo Magomeni.
Akizungumzia kuhusu uwanja huo, Sitta alisema utagharimu Sh2.7 bilioni hadi kukamilika ni kati ya miradi mitatu ambayo ilipitishwa katika bajeti ya mwaka 2019/2020 na baraza la madiwani.
Meya huyo aliendelea kueleza kuwa uwanja huo utakuwa ni chanzo kimojawapo cha mapato kwa Manispaa hiyo kwa kuwa ndani yake kutakuwa na maduka 50, mabweni na pia watakuwa wakikodisha kwa timu na mashindano mbalimbali.
Luteni kanali, Luoga amesema ujenzi wa uwanja huo awali ungejengwa kwa miezi nane, lakini sasa utakamilika ndani ya miezi sita.
"Kama Jeshi tumeona muda ulipangwa na Manispaa kukamilika kwa uwanja huo kuwa ni miezi nane, lakini kwetu niwahakikishie utaisha ndani ya miezi sita kikubwa ni kuletewa vifaa vyote vinavyohitajika kwa wakati kwa kuwa rasilimaliwatu tunayo ya kutosha," amesema.
Alibainisha kuwa kukamilika kwake utakuwa na uwezo wa kuchukua watu takribani 20,000 kwa wakati mmoja.
Mwenyekiti wa Timu ya KMC FC, Heri Nassoro amesema ujenzi wa uwanja huo kwao ni faraja kwa kuwa utawapunguzia gharama za kutafuta mahali pa kuweka kambi na kufanyia mazoezi walizokuwa wakiingia.