Ubingwa Yanga washindwe wao tu!

Yanga ishindwe yenyewe kileleni

Muktasari:

Yanga inatarajia kushuka uwanjani tena kesho kuivaa JKT Tanzania Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Yanga imejihakikishia kukaa kileleni kwa muda hadi kesho itakaposhuka tena uwanjani kuivaa JKT Tanzania katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Miamba hiyo ya soka nchini iliibuka na ushindi wa bao 1-0 juzi dhidi ya Azam FC, shukrani kwa bao la kiungo mshambuliaji, Deus Kaseke, likiwa bao lake la kwanza Ligi Kuu msimu huu.

Katika mchezo huo wa juzi, Yanga ilikuwa na nafasi ya kupata mabao zaidi hasa kipindi cha kwanza, lakini ilishindwa kutokana nma kutokuwa makini kwa washambuliaji wake waliokuwa wakiongozwa na Ditram Nchimbi, aliyesaidiwa na Tuisila Kisinda na Yacouba Sogne.

Sogne alikuwa na nafasi ya kufanya Yanga kuwa na uhakika tangu kipindi cha kwanza, lakini aliunganisha vibaya krosi ya beki wa kulia, Kibwana Shomary, huku pia krosi ya pili akishindwa kuifikia kwa kichwa.

Balaa zaidi lilikuwa klatika dakika nne za nyongeza aliposhindwa kutumia makosa ya kipa David Mapigano aliyegongana na beki wake na mpira kudondoka mbele yake, lakini alishindwa kuunganisha kwenda katika lango lililokuwa tupu.

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze anaonekana kuwa katika kazi ya ziada kuimarisha kikosi chake, hasa katika eneo la ushambuliaji, ambalo bado halimpi matokeo chanya ya kumaliza mchezo mapema.

Kwa uongozi wa bao 1-0, Yanga inalazimika kutumia nguvu nyingi katika dakika 20 za mwisho kwenye kila mchezo kujilinda zaidi, kwani uongozi huo mwembamba unaacha matumaini kwa wapinzakutaka kusawazisha.


Dube aumia, asafirishwa

Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube aliyeumia katika mchezo huo wa juzi dhidi ya Yanga atasafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi.

Dube aliumia baada ya kudondoka vibaya alipokuwa akiwania mpira wa juu na beki wa Yanga na kuumia mfupa mdogo wa mkono wa kushoto na kushindwa kuendelea na mchezo dakika ya 15, nafasi yake ilichukuliwa na Richard Djodi dakika 24.

Kupitia mitandao ya kijamii ya Azam, iliandika: “Dube raia wa Zimbabwe, aliumia dakika ya 15 kwa kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto (Ulnar), mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho.

“Ataondoka nchini Novemba 29, kwa Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ), atatibiwa kwenye hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, chini ya daktari bingwa wa mifupa, Robert Nicolas.”

Nyota huyo ndiyo mfungaji bora wa kikosi cha Azam hadi sasa, akiweka kambani mabao sita, moja nyuma ya kinara wa mabao Ligi kuu, John Bocco wa Simba.

Daktari wa Yanga, Shecky Mngazija alisema majeraha ambayo ameyapata Dube, inategemea aina ya matibabu ambayo atapatiwa ndiyo itafahamika muda gani anaweza kuwa nje ya uwanja.

Kibwana naye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia kipindi cha pili na nafasi yake kuingia, Said Juma Makapu.

Haijafahamika kama nyota huyo anaweza kuukosa mchezo wa kesho kutokana na kutokuwa matibabu zaidi baada ya kutoka uwanjani kipindi cha pili.

Wakati Yanga ikiikaribisha JKT Tanazania kesho, Azam FC itacheza Jumapili kwa kuivaa Biashara United uwanja wa Karume, Musoma.