Ubingwa wa Yanga wamuibua Ramovic

Muktasari:
- Ramovic, ambaye aliiongoza Yanga katika mzunguko wa kwanza wa msimu wa 2024/25 kabla ya kutimkia CR Belouizdad amesema anatambua ukubwa wa mafanikio ya Yanga msimu huu na amesisitiza ubingwa huo ni heshima kwa kila aliyewahi kuwa sehemu ya klabu hiyo.
BAADA ya Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mfululizo, aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Sead Ramovic amevunja ukimya na kutoa pongezi kwa klabu hiyo, huku akieleza fahari yake kwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo.
Ramovic, ambaye aliiongoza Yanga katika mzunguko wa kwanza wa msimu wa 2024/25 kabla ya kutimkia CR Belouizdad amesema anatambua ukubwa wa mafanikio ya Yanga msimu huu na amesisitiza ubingwa huo ni heshima kwa kila aliyewahi kuwa sehemu ya klabu hiyo.
"Hongera kwa klabu pendwa ya Young Africans kwa Rais Hersi, wachezaji, benchi la ufundi na timu nzima ya kiufundi kwa kutwaa taji la ligi,” alisema Ramovic.
Kocha huyo alisisitiza, mafanikio ya Yanga si ya bahati nasibu bali ni matokeo ya kazi kubwa na mshikamano wa hali ya juu ndani ya timu, huku akikiri kuwa bado ana kumbukumbu nzuri za muda wake Jangwani.
"Ninajivunia na kufurahia kuwa sehemu ya safari hii, nikichangia kwa mchango mzuri na mafanikio wakati wa muda wangu na timu.”
Katika msimu ambao ushindani ulikuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni, Yanga walimaliza kileleni wakiwa na pointi 82, wakiwazidi Simba kwa pointi nne.
Ramovic pia amempongeza Kocha wa Simba, Fadlu Davids, akimtaja kama mmoja wa makocha bora aliowahi kumkabili kwenye ligi na ushindani dhidi yake ulifanya ubingwa wa Yanga kuwa na thamani ya kipekee.
“Kushinda taji hili muhimu hasa dhidi ya kocha bora kama Fadlu Davids, ambaye kazi yake, akili yake, na utu wake vinajieleza wazi ni mafanikio ya kuheshimika sana,” aliongeza.
Ramovic, ambaye aliondoka Yanga akiwa hajapoteza mechi yoyote kwenye ligi, anatajwa aliweka msingi thabiti uliowezesha timu kuendelea kuwa imara hadi mwisho wa msimu, chini ya Kocha Miloud Hamdi aliyemrithi.
Yanga imetwaa ubingwa huo kwa kuongoza karibu vipengele vyote vya ligi; ikijivunia safu ya ulinzi iliyoruhusu mabao machache, safu kali ya ushambuliaji pamoja na nidhamu ya kimchezo.
Katika salamu zake za pongezi, Ramovic alihitimisha kwa kusema:
"Huu ni wakati wa kujivunia kwa kila mmoja aliye karibu na Yanga. Naomba klabu iendelee kukua na kung’ara katika kila jukwaa itakalokanyaga.”
Ubingwa wa Yanga uliotokana na kuvuna jumla ya pointi 82 katika mechi 30, ikishinda 27 na kutoka sare moja na kupoteza mbili, ulichangiwa na makocha watatu akiwamo Miguel Gamondi aliyeiongoza katika mechi 10, akishinda nane na poteza mbili, kisha Ramovic akaiongoza katika mechi sita zote akishinda kabla ya kutimkia Algeria.
Kisha katika mechi moja dhidi ya KenGold, Abdihamid Moallin alisimama kama kocha kushinda 6-1 na kukabidhi kijiti kwa Miloud Hamdi aliyemalizia mechi 13, akishinda 12 na kutoka sare moja na sasa kocha huyo anajiandaa katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars.