Ubingwa au kusalia Ligi? Simba na Mbeya City zakutana mechi ya uamuzi
Muktasari:
- Simba yenye pointi 61 katika nafasi ya pili ipo pointi mbili nyuma ya Yanga, inatarajia kushuka uwanjani leo Jumatano kuwakabili Mbeya City waliopo nafasi ya 13 kwa pointi 25, mchezo utakaopigwa saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ikiwa ni mechi ya kwanza ya Simba kupigwa mchana.
LICHA ya kukiri ugumu wa ligi na vita ya ubingwa msimu huu, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema kwa sasa anatazama michezo yake iliyobaki kuhakikisha hapotezi mechi yoyote, huku Mbeya City wakitamba kutibua mipango yao ili wabaki kwenye ligi.
Simba yenye pointi 61 katika nafasi ya pili ipo pointi mbili nyuma ya Yanga, inatarajia kushuka uwanjani leo Jumatano kuwakabili Mbeya City waliopo nafasi ya 13 kwa pointi 25, mchezo utakaopigwa saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ikiwa ni mechi ya kwanza ya Simba kupigwa mchana.
Timu hizo zinakutana ikiwa Simba inajivunia rekodi nzuri dhidi ya wenyeji hao, kwani katika michezo 10 wameshinda mechi tisa na sare moja ikiwamo mchezo wa mwisho kukutana Desemba 4, City walilala mabao 3-0.
Akizungumza jijini hapa, Barker amesema anafahamu ugumu wa mchezo huo kutokana na matokeo ya timu zote na kwa sasa anaangalia zaidi mechi zake kuhakikisha wanashinda.
Kuhusu vita ubingwa msimu huu, kocha huyo amesema hawajakata tamaa kwa kuwa ligi haijaisha na presha ni kubwa akitambia kikosi chake kuwa fiti na kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi nne zilizobaki.
“Kwenye msimamo upinzani ni mkali lakini hatuna sababu yoyote ya kutoshinda mchezo dhidi ya Mbeya City, tunajua ugumu wake lakini umuhimu wa pointi tatu, vijana wako tayari kwa mchezo huu.
“Ratiba ni ngumu ila tunaendelea kupambana kulinda ushindi ili kuwania ubingwa msimu huu, kimsingi tunapambana kushinda mechi zetu bila kuangalia wapinzani wakoje au wanapata matokeo gani,” amesema kocha huyo ambaye hajapoteza mchezo wowote kwenye ligi hadi sasa.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga ambaye ana uzoefu wa kutosha kwenye ligi, alisema mchezo huo utakuwa wa mbinu na ufundi, akieleza kuwa wanafahamu ugumu wake ila
hesabu zao ni kushinda mechi hiyo ili kujiweka nafasi nzuri ya kubaki kwenye ligi.
Alisema kwa sasa hakuna njia mbadala zaidi ya kushinda kila mchezo wakianza na Simba kesho kuhakikisha wanajiweka pazuri, akifafanua kuwa makosa yaliyoonekana mechi zilizopita wameyafanyia kazi na sasa wanaingia uwanjani wakiwa fiti kwa asilimia kubwa.
“Tunajua tunakutana na timu bora Afrika, lakini tumejipanga kupata ushindi na hatuna njia mbadala zaidi ya kupata pointi tatu ili kujinasua nafasi za chini, vijana wako timamu kiakili na kiufundi kwa ajili ya mechi hiyo.”