Twiga Stars yashindwa kutamba kwa Mkapa

TIMU ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars imekubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka  kwa Namibia katika mchezo wa kufuzu michuano ya AFCON mwakani nchini Morocco.

Bao la kusawazisha kwa Stars kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Stumai Abdallah limeshindwa kuipatia sare timu hiyo baada ya Namibia kupata bao la utangulizi dakika ya 22, kupitia kwa kiungo anayechezea klabu ya Sevilla ya nchini Hispania Zenatha Coleman.

Kipindi cha pili Namibia walifanya mabadiliko ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji baada ya kuwatoa Kotjipati Veweziwa na Memory Ngonda na nafasi zao kuchukuliwa na Millicent Feilicity na Meltret Ujamba.

Mabadiliko hayo yalileta manufaa kwa wageni kwani dakika ya 62, kiungo Zenatha Coleman aliipatia bao la pili na la ushindi Namibia baada ya kupiga pigo huru lililomshinda golikipa wa Stars Janeth Simba.

Stars ilifanya mabadiliko dakika ya 66, kwa kumtoa mshambuliaji Mwanahamis Omary ambaye alishindwa kuonyesha makali yake toka mwanzo wa mchezo na nafasi yake ikichukuliwa na Irene Kisisa.

Namibia wangeweza kupata bao la tatu baada ya Meltret Ujamba kupiga shuti lililoenda nje ya lango la Stars baada ya kusalia na golikipa Janeth Simba.

Licha ya jitihada za Stars kulishambulia lango la Namibia ila walishindwa kusawazisha bao hilo na kushindwa kutumia vyema faida ya Uwanja wa nyumbani.

Kocha wa Twiga Stars Bakari Shime 'Mchawi Mweusi' ana kazi kubwa ya kufanya kupindua matokeo haya wakati kikosi hicho kitakaporudiana nchini Namibia Oktoba 23.