Twiga Stars yaitaka Olimpiki

Muktasari:

  • Shime ambaye mwaka jana aliiongoza timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Girls' kushiriki fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika India, alisema kuwa maandalizi ambayo wanaendelea kuyafanya, yanawapa imani kuwa safari hii wataweka historia ya kushiriki kwa mara ya kwanza michezo ya Olimpiki.

SIKU moja baada ya kupangwa kukutana na Congo katika raundi ya kwanza ya kufuzu michezo ya Olimpiki 2024 huko Ufaransa, kocha wa timu ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars', Bakari Shime ametamba kuwa watahakikisha wanatimiza lengo.

Shime ambaye mwaka jana aliiongoza timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Girls' kushiriki fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika India, alisema kuwa maandalizi ambayo wanaendelea kuyafanya, yanawapa imani kuwa safari hii wataweka historia ya kushiriki kwa mara ya kwanza michezo ya Olimpiki.

"Droo tumeiona na kiuhalisia tunakutana na timu ngumu na nzuri ambayo imepiga hatua katika soka la wanawake. Katika mashindano haya, lengo kuu ni kufuzu na ili ufanye hivyo hauwezi kukutana na timu rahisi tu. Lazima ukutane na ugumu ambao unatakiwa kuushinda ili ufanikishe malengo yako.

"Kwa upande wetu hatuna wasiwasi wowote kwa sababu tumekuwa katika maandalizi ya muda mrefu na tuna muendelezo mzuri wa vijana ambao tunawaandaa kutoka chini hivyo tulishajiandaa kukutana na yoyote ambaye tungepangiwa naye," alisema Shime.

Katika droo ya kuwania kufuzu fainali hizo iliyochezeshwa juzi kwenye makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Twiga Stars imepangwa kukutana na Congo katika raundi ya kwanza ikianzia ugenini na kumalizia nyumbani na mshindi wa mechi mbili baina yao, atakutana na Botswana kwenye raundi ya pili.

Ikiwa itapenya hapo, Twiga Stars itaingia katika raundi ya tatu ambayo itahusisha timu nane na mwishoni ni raundi ya nne ambayo washindi wake wawili watafuzu kushiriki mashindano ya soka ya Olimpiki kwa wanawake.

Kwa mujibu wa kalenda ya CAF ya mashindano hayo, mechi za raundi ya kwanza zitachezwa kuanzia Julai 10 hadi 18 wakati zile za raundi ya pili zimepangwa kuchezwa kati ya Oktoba 23 hadi 31 mwaka huu.

Mechi za raundi ya tatu zitachezwa mwakani kati ya Februari 19 hadi 28 na raundi yamwisho itakayotoa washindi wawili itafanyika kati ya Aprili Mosi hadi tisa mwakani.