Twiga Stars, Namibia hakuna mbabe

DAKIKA 45, za kipindi cha kwanza zimetamatika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars kufungana bao 1-1, dhidi ya Namibia katika mchezo wa kufuzu (AFCON) Mwakani nchini Morocco.

Bao la Namibia limefunga dakika ya 22, na kiungo Zenatha Coleman baada ya walinzi wa Stars kufanya makosa nje ya eneo la 18.

Baada ya bao hilo Stars ilianza kulishambulia lango la Namibia huku umakini ukikosekana wa kumalizia nafasi zilizokuwa zimepatikana.

Beki wa kushoto wa Stars Enekia Kasonga alishindwa kuisawazishia bao Stars dakika ya 29, baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Namibia.

Dakika 38, Kocha Mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime alifanya mabadiliko ya kumtoa beki wa kati Clara Luvanda na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Aisha Masaka ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya kuelekea mapumziko, Stars ilipata bao la kusawazisha kupitia kwa kiungo mshambuliaji Stumai Abdallah baada ya kupiga mpira uliomshinda golikipa Melisa Matheus.