Tshishimbi awapa Simba SC masharti, Yanga wajipanga upyaa

Muktasari:
Simba imekuwa ikimhitaji Tshishimbi kwa ajili ya kusaidiana na Jonas Mkude, kama hitaji la Kocha Sven Vaderbroeck aliyetaka pia asajiliwe beki wa kati mmoja matata na straika mkali kuliko Meddie Kagere na John Bocco ili chama lao litishwe kwenye michuano ya kimataifa.
MASHABIKI wa Yanga hawana amani kwa sasa. Kwanza bado hawajajua hatma ya Kampuni ya GSM katika kuendelea kuwapa raha nje ya mkataba walioingia na klabu yao, lakini pia kelele za watani wao kwamba wanambeba nahodha Papy Kabamba Tshishimbi zinawachanganya kinoma.
Hata hivyo, jambo la kufurahisha ni kwamba, mabosi wa klabu hiyo wamejipanga ili kumzuia nahodha huyo, asivuke maji na kutua upande wa pili, lakini pia kule Msimbazi, kiungo huyo amewatega katika mambo matatu ili kumvuta wakakinukishe na Jonas Mkude pale Simba.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa rafiki wa karibu wa nyota huyo kutoka DR Congo aliyewahi kukipiga Mbabane Swallows ya eSwatini, ni kwamba Tshishimbi amewataka Simba wasubiri kwanza kuona muda ambao amewapa Yanga umalizike na kama hataona kitu chochote, basi atarejea katika meza ya mazungumzo na Wekundu hao.
Rafiki huyo aliongeza, mbali na sharti hilo pia kiungo huyo amewaambia Simba kumwandalia mkataba wa Dola 70,000(160 milioni) huku mshahara wa Dola 5,000 (sh 11.5 milioni) ili asaini.
Hata hivyo, Simba inaelezwa iliona ugumu katika sharti hilo la pili wakikubaliana na kiwango cha mshahara pekee huku dau la usajili wakitaka lipungue.
“Aliwaambia hivyo, sasa unajua Tshishimbi kuna watu anawaheshimu sana ndani ya Yanga ndio maana amewaambia Simba wasubiri kwanza kuona kipi kitaendelea kati yake na mabosi wake wa sasa na hao watu ndio wanaomzuia asifanye uamuzi wowote,” alisema rafiki huyo aliyeombwa kuhifadhiwa jina lake.
“Simba inakubaliana na hicho kiwango cha mshahara, lakini hapo kwenye dau la usajili bado hawajakubali na yeye hataki kushusha sasa tusubiri tuone kipi kitatokea.”
Simba imekuwa ikimhitaji Tshishimbi kwa ajili ya kusaidiana na Jonas Mkude, kama hitaji la Kocha Sven Vaderbroeck aliyetaka pia asajiliwe beki wa kati mmoja matata na straika mkali kuliko Meddie Kagere na John Bocco ili chama lao litishwe kwenye michuano ya kimataifa.
YANGA YAJIPANGA
Filamu hiyo ya Tshishimbi na Simba, Yanga nao wanaifuatilia kwa karibu ambapo taarifa kutoka ndani ya timu hiyo ni kwamba tayari mabosi wa klabu hiyo wanajipanga kuyafanyia kazi maombi ya Kocha Luc Eymael aliyewaambia hataki kuona kiungo huyo anaikimbia timu yake.
Walichokifanya Yanga ni kukutana fasta na tayari wameshajadiliana jinsi ya kumbakisha kiungo huyo na inaelezwa Tshishimbi ameshaanza kuitwa katika vikao vya kuongeza mkataba mpya.
“Kuna kiongozi wa Yanga alienda kuonana naye wikiendi hii (wikiendi iliyopita) sasa tusubiri kuona kipi ataelezwa huko maana naona Yanga nayo imeamka kutokana na kauli ya kocha wao (Eymael) ambaye pia amempigia mchezaji mwenyewe akimwambia bado anamuhitaji kikosini.”
Tshishimbi mara kadhaa amekuwa akisisitiza kwamba, mkataba wake umebakiza muda mchache kabla ya kumalizika na ameshafuatwa na watu wa Simba mara kadhaa ili wamsajili, lakini anaipa heshima kubwa klabu yake iliyomleta Tanzania kama mazungumzo yao yataenda salama.
“Sina tatizo. Mimi bado ni mali ya Yanga hata kama mkataba unaniruhusu kuzungumza na klabu yoyote na ni kweli Simba imenitafuta tena sio mara moja,” alikaririwa Tshishimbi.