Try Again atuliza mashabiki Simba

Muktasari:

  • Try Again alisema kwa sasa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanapaswa kuiunga mkono timu yao, kwa vile mambo matamu yanarudi baada ya kutibuka hivi karibuni hasa baada ya kipigo cha Yanga.

KIKOSI cha Simba kipo angani kuelekea Botswana kuwavaa Jwaneng Galaxy Jumamosi. Mabosi wa klabu hiyo wamewahakikishia raha inarejea baada ya kutua kocha mkuu mpya, Abdelhak Benchikha.

Benchikha anachukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye sasa yuko Saudia akipunga upepo. Kocha huyo aliweka wazi kwamba yuko tayari kufanya kazi na mchezaji yoyote yule ambaye atajituma na kufanya vizuri na ndio maana anajipa muda wa kumuangalia kila mchezaji nini anakifanya katika nafasi anayoicheza, lakini akizingatia suala la nidhamu ni mkali kwa anayekiuka taratibu anazoziweka kikosini.

“Mimi ni mpambanaji siogopi changamoto ya aina yoyote ile, mchezaji anayejituma nitafanya naye kazi najua sasa hivi timu inapitia kipindi kigumu naamini kwa pamoja tunaweza kuirejesha katika hali nzuri,” alisema Benchikha, lakini Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema, viongozi wana imani kubwa na kocha huyo na ndio maana wamemleta kuinoa timu yao.

Try Again alisema kwa sasa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanapaswa kuiunga mkono timu yao, kwa vile mambo matamu yanarudi baada ya kutibuka hivi karibuni hasa baada ya kipigo cha Yanga.

“Tumeongea muda mwingi na kocha wetu, tumemuahidi kumpa ushirikiano wa asilimia 100 kuhakikisha timu inafanya vizuri,” alisema Try Again aliyeongeza kuwa, wanatambua mashabiki wao hawana furaha na timu yao kutokana na aina ya matokeo ambayo wanayapata akikiri ni kipindi cha mpito tu. “Hata kocha tumemwambia ajitahidi kuhakikisha mamilioni ya mashabiki wetu wanapata kile ambacho wanakihitaji kuona timu inafikia,” alisema.


YAPEWA MBINU

Mtaalam wa soka, Jonas Tiboroha alisema, ili Simba ikaambulie walau pointi moja dhidi ya Jwaneng inatakiwa kupaki basi ikijifanya kushambulia itakachokipata haitoamini jambo lililowaponza wababe wao Wydad waliolala 1-0 nyumbani mbele ya timu hiyo ya Botswana iliyowahi kuing’oa Simba kwenye mechi za mchujo za CAF misimu miwili iliyopita.

Tiboroha alisema benchi la Simba liwajaze wakabaji wote, Shomary Kapombe, Israel Mwenda, Che Malone Fondoh, Kennedy Juma, Henock Inonga, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute wakakabe na sio kushambulia, kwani wakijichanganya wanaweza kujitibulia kama Wydad.

“Jwaneng waliwasumbua nakumbuka waliwaondoa na wakati huo Simba iko vizuri, kwa Simba haipo kivile, hivyo wakipaki basi tu hakuna namna ni ushauri tu, wakiwa wanajipanga kufanyia kazi mapungufu katika dirisha dogo,” alisema Tiboroha aliyeamua kukaa mbali na soka kwa sasa.

Nyota wa zamani wa Simba, Fikiri Magoso alisema, timu hiyo inapitia katika wakati mgumu hivyo wenye kurejesha furaha ni wachezaji kuhakikisha wanapambana na kutambua thamani ya uwepo wao Msimbazi.  “Hakuna namna ni wachezaji kujitoa,” alisema Magoso.