Tizi tano zinajenga mwili wako fresh tu

Muktasari:

Yapo mazoezi ambayo yanakubalika na wataalamu wa tiba za michezo na mazoezi ya viungo kuwa ndio yanayoufanya mwili kujengeka kutokana na uwezo wa kushughulisha misuli ya mwili.

BAADA ya wiki mbili zilizopita kuwapa ufahamu kuhusu lishe na ratiba ya mlo wa siku kwa wanasoka leo nitawapa ufahamu wa mazoezi yanayojenga mwili si tu kwa wanamichezo, bali pia kwa watu wakawaida.

Mwanadamu wa kawaida na wanamichezo wanahitaji mazoezi bora ambayo yanayoujenga mwili na kuufanya uwe imara na afya njema.

Mazoezi ni nyenzo ya msingi katika kukabiliana na uzito mkubwa na unene uliokithiri, hivyo kusaidia kuepukana na magonjwa yasiyombukiza yanayotokana na unene uliokithiri ikiwamo kisukari, magonjwa ya moyo na kiharusi.

Mwanadamu hasa kwa mwanaume kuwa na mwili wenye mwonekano mzuri ulio na misuli imara na iliyojengeka ni jambo ambalo linapendwa lakini si kila zoezi linaweza kuujenga mwili wote.

Wanadamu hasa vijana huwa na hulka ya kupenda kuwa na mwonekano mzuri unaovutia pale wanapovaa mavazi ya kisasa.

Maumbo hayo maarufu kama sexiest body ndiyo yanayompa umaarufu mchezaji bora mara tano duniani, Cristiano Ronaldo.

Mchezaji huyu amewahi kupewa tuzo maarufu na Jarida la Men’s Health la Marekani ya Mwanaume Bora wa Mwaka mwenye umbo lenye kujengeka na kuvutia.

Wapo vijana wengi ambao hubeba vyuma vizito kiholela ili kuujenga miili yao pasipo kufahamu ni aina gani ya mazoezi yanayoweza kujenga miili yenye mvuto.

Yapo mazoezi ambayo yanakubalika na wataalamu wa tiba za michezo na mazoezi ya viungo kuwa ndio yanayoufanya mwili kujengeka kutokana na uwezo wa kushughulisha misuli ya mwili.

Mazoezi haya endapo mwanadamu atayafanya mara kwa mara humfanya kuwa na mwili imara uliojijenga.

Zoezi linaloshika namba moja kwa kujenga mwili huwa ni kuogelea. Zoezi hili linaujenga mwili kwani kuogelea kunahusisha misuli mingi zaidi kuanzia miguu, kiwiliwili, mikono na kichwa.

Jaribu kuwatazama wavuvi, wapiga mbizi, wanamichezo waogeleaji utagundua wamejengea mwili mzima.

Zoezi la pili ambalo linashika nafasi ya pili kwa kujenga mwili huwa ni kucheza muziki, lakini sio muziki laini kama ilivyo bluzi au taarabu asilia.

Muziki kama wa dansi, Afro, House, Hot Funky, Pop na ngoma za utamaduni. Muziki wa aina hii uchezaji wake unahusisha kuchezesha misuli mingi mwilini, hivyo kumfanya mchezaji kuwa na misuli imara.

Miaka ya nyuma Mwanamziki wa zamani wa Rap, Mc Hammer alikuwa akipungua kilo mbili kila baada ya kutoka katika tamasha alililotumbuiza hii ni kutokana na mwili wake kutumia misuli mingi wakati wa kucheza mitindo yake.

Zoezi linaloshika namba tatu huwa ni kukimbia, mwanadamu anapokimbia huweza kuhusisha misuli ya mwili mzima. Ukiwatizama wanariadha wengi duniani wana miili imara yenye misuli iliyojijenga vema.

Upo ushahidi wa kitafiti unaonyesha ufanyaji wa zoezi hili kuchangia mamilioni ya wakimbiaji kuwa na miili iliyojengeka huku wakiishi maisha marefu zaidi.

Michezo kama sarakasi, michezo ya karate, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mchezo wa rugby yenyewe ndio inashika namba nne kwa kujenga misuli na kumfanya mwanadamu kuwa imara kimwili na kiafya.

Zoezi namba tano huwa ni kutembea nako ni mojawapo ya zoezi ambalo linahusisha misuli mingi ya mwilini, kutembea umbali mrefu ndiko haswa kunakojenga mwili.

Mtindo huu ndio unaowafaa watu wenye umri mkubwa wanaohitaji kujenga mwili wenye afya njema.

Utahitajika kutembea umbali wa wastani angalau kilometa mbili kwa siku katika siku tano za wiki huku ukitembea na kutupa mwili na mikono ili kuishughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi ndio chanzo cha kuwa na mwili imara wenye afya njema, hivyo kuepukana na maradhi yasiyoambukiza ikiwamo kisukari cha aina ya pili, maradhi ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.

Hii ndiyo sababu inayochangia mamilioni ya wanamichezo duniani pamoja na wafanya mazoezi mepesi ya mara kwa mara kuishi kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na wasiofanya mazoezi.

Lakini swali la msingi zaidi je, mazoezi haya yafanyike kwa muda gani ili kupata matokeo chanya? Kwa kifupi inashauriwa mazoezi haya yafanyike kwa siku dakika 30-60 katika siku 5 za wiki.

Vilevile inashauriwa kufuata mwenendo na mitindo bora wa kimaisha ikiwamo mlo kamili uliozingatia kanuni za lishe.

Mwenendo na mitindo mibaya ya kimaisha inayoweza kuchangia kutoweza kujenga mwili hata kama unafanya mazoezi haya ni pamoja ulaji holela wa vyakula vyenye mafuta mengi, wanga na sukari nyingi, unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji tumbaku.

Vyakula hivi ambavyo hupatikana zaidi mitaani, katika migahawa ya kisasa hasa ya Kimagharibi, vyakula vya kusindika hasa vile vinavyuouzwa katika maduka makubwa (supermarkets).

Vyakula hivi huchangia watu kunenepa na kuwa na uzito au unene uliokithiri, hivyo kuharibu ule mwonekano wa ukakamavu wa mwili kutokana na mrundikano wa mafuta mengi.

Kama unapenda kuwa na mwili uliojengeka zingatia mojawapo ya mazoezi haya au fika katika vituo vya mazoezi kwa ushauri zaidi.

Jipangie ratiba ya kufanya mazoezi haya mara kwa na kuwa sehemu ya maisha yako kwani si tu yanaujenga mwili kimazoezi, bali pia kukufanya kuwa na afya njema.