Timu 16 kukiwasha Kagame Cup 2024, mashindano kuanza rasmi Julai 6

Muktasari:

  • Timu tatu alikwa, TP Mazembe (DR Congo), Nyasa Big Bullets (Malawi) na Red Arrows FC ya Zambia zote zimethibitisha ushiriki wao kujiunga na timu 13 nyingine kutoka Ukanda wa CECAFA.

Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limetangaza kwamba mashindano ya CECAFA Kagame Cup mwaka 2024 yatafanyika Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Julai 6 hadi 22 mwaka huu ikizishirikisha timu 16.

Timu tatu alikwa, TP Mazembe (DR Congo), Nyasa Big Bullets (Malawi) na Red Arrows FC ya Zambia zote zimethibitisha ushiriki wao kujiunga na timu 13 nyingine kutoka Ukanda wa CECAFA.

Awali, mashindano hayo yalipangwa kufanyika kuanzia Julai 20 hadi Agosti 4 mwaka huu nchini Tanzania, lakini kutokana na ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuonyesha kuanza Agosti, CECAFA wameona mashindano yao yaanze mapema na kumalizika siku chache kabla ya kuanza kwa mtifuano wa michuano ya CAF ngazi ya klabu msimu wa 2024/2025.

"Mashindano haya yatasaidia timu zetu katika ukanda huu kujiandaa vizuri kabla ya msimu wa CAF Champions League na CAF Confederation Cup 2024/2025 ambao unaanza mwezi Agosti. Kuwa na timu kubwa kutoka DR Congo, Malawi na Zambia pia kutapa msisimko kwenye mashindano yetu na kutoa changamoto halisi kwa timu zetu," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, John Auko Gecheo.

Kutokana na hilo, michuano ya Cecafa Senior Challenge Cup mwaka 2024 ambayo yanahusisha timu za taifa iliyokuwa imepangwa kufungua Kalenda ya CECAFA kuanzia Juni 29 hadi Julai 14 mwaka huu, imefutwa ili kuwapa wachezaji muda zaidi wa kujiandaa na klabu zao kabla ya Cecafa Kagame Cup.

Timu zitakazoshiriki michuano ya Cecafa Kagame Cup ni: Vital’O (Burundi), APR (Rwanda), El Merreikh, Al Hilal, Hai El Wadi (Sudan), Yanga, Simba, Azam, Coastal Union (Tanzania), Gor Mahia (Kenya), SC Villa (Uganda), JKU SC (Zanzibar), El Merreikh FC-Bentiu (Sudan Kusini), Nyasa Big Bullets (Malawi), TP Mazembe (DR Congo) na Red Arrows (Zambia).