Timbe aingia na gia mpya Yanga

Kikosi cha Yanga kikijiandaa kwa ligi ya Vodacom msimu huu, na mechi ya ngao ya hisani itakayochezwa hivi karibuni, chini ya usimamizi wa kocha mkuu Sam Timbe
DORIS MALIYAGA na OLIVER ALBERT KOCHA Sam Timbe haishi mambo. Sasa ametua Yanga na gia mpya ambayo amemkabidhi fowadi wake Mghana Kenneth Asamoah na kufanya siri kubwa huku akiwapiga wachezaji mchakamchaka kila asubuhi. Simba na Yanga zitachuana Agosti 17 kwenye mechi ya Ngao ya Hisani ndani ya Uwanja wa Taifa. Yanga bado ipo kwenye maskani yake yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam huku Simba ikiendelea na mazoezi makali mjini Zanzibar. Timbe kama ilivyo kwa wachezaji wake ameonekana kupania kuifunga Simba lakini akasisitiza kuwa mbinu zake na Asamoah zitabaki kuwa siri nzito. Asamoah ndiye mfungaji wa bao pekee la ushindi lililowapa Yanga ubingwa wa Kombe la Kagame katika mechi ya fainali. Alifunga bao hilo akiingia dakika 15 za mwishoni katika mechi hiyo iliyochezwa dakika 120. Katika mazoezi ya jana Jumatatu katika Uwanja wa Kaunda, jijini Dar es Salaam, Timbe alitumia muda mwingi kuzungumza na Asamoah na ilifika muda akamwita pia beki wa pembeni, Oscar Joshua na kutumia dakika kadhaa kuwafundisha kwa ishara mbalimbali. Mwanaspoti ilishuhudia tukio hilo ambalo Timbe alitumia mikono yake kumpa mbinu Mghana huyo. Kocha huyo alificha kitu na kumwambia Asamoah anataka ampe zawadi. Alimnyooshea mikono yake na kumwelekeza kuchagua mkono wenye zawadi, Asamoah alichagua mkono wa kulia na akakuta kulikuwa na jiwe. Timbe sasa kwa kutumia jiwe lile alianza kumpa maelekezo Asamoah. Timbe aligoma kuifafanulia Mwanaspoti kitendo kile kilikuwa na maana gani. Alipoulizwa alisema;"íNdiyo hivyo ulivyoona, mambo haya ni siri yangu, siwezi kuweka wazi mbinu zangu ili wapinzani wasizijue, kama naandaa mbinu na kuelekezana na wachezaji wangu kamwe siwezi kukwambia wapinzani watajua nini tunafanya. Asamoah alisema; ëíAliniita na kuniambia nichague akiwa ameficha jiwe mkononi, nikachagua, baada ya hapo akanielekeza mambo fulani, zilikuwa mbinu za kimichezo ambazo nilitakiwa kuzifanya nikiwa uwanjani ni hivyo tu hakukuwa na jingine. Kwa upande wa Oscar alisema kuwa; ëíIlikuwa hivyo, mwalimu alikuwa akituelekeza mambo tu ya uwanjani. MAZOEZI Kocha huyo amekuwa akiwapa mazoezi ya saa tatu kila asubuhi kuanzia saa 2 hadi saa 5 ili kuwaweka fiti zaidi, amekuwa akiwafundisha mazoezi ya kumiliki mpira, pasi ndefu na fupi pamoja na jinsi ya kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza. Timbe anataka timu hiyo itulize mpira chini na si kubutua au kushambulia bila mipango. "Nimefika jana (juzi) Jumapili na nimeanza mazoezi na timu kujiandaa na Ligi Kuu na mechi dhidi ya Simba na kama unavyoona ninachokazania timu itulize mpira, soka la butua butua halina maana, mpira ni magoli na burudani," alisema na kusisitiza kuwa suala la kambi ni juu ya uongozi. Wachezaji waliohudhuria mazoezi jana Jumatatu ni Godfrey Taita, Jerry Tegete, Juma Seif Kijiko, Shadrack Nsajigwa, Pius Kisambale, Ibrahim Job, Zubery Ubwa, Nadir Haroub `Cannavaro', Nurdin Bakari, Bakari Mbegu, Davies Mwape, Fred Mbuna, Godfrey Bonny, Abuu Ubwa, Shamte Ali, Said Mohamedy, Kigi Makasy, Idrisa Rashid, Julius Mriope, Kenneth Asamoah na Oscar Joshua. Haruna Niyonzima 'Fabregas' alitua jana Jumatatu mchana kutoka Rwanda wakati Hamis Kizza alitarajiwa kuwasili saa moja usiku jana hiyo hiyo kutoka Uganda. WATORO Timbe amesisitiza kuwa ambao hawatahudhuria mazoezi hadi leo Jumanne bila ruhusa maalumu watakatwa mshahara. Wachezaji 22 tu ndio waliohudhuria mazoezi jana Jumatatu ukiondoa Kizza na Haruna na Shabaan Kado aliyeko timu ya Taifa ya vijana wakati Rashid Gumbo hajulikani alipokwenda. Mwanaspoti ilishuhudia baadhi ya viongozi wa Yanga akiwemo msemaji Luis Sendeu wakiulizana; 'Gumbo yuko wapi' kwani hakuonekana mazoezini. Lakini Timbe alipoulizwa mbona wachezaji wengine hawaonekani akiwemo Gumbo; alijibu "Ninachojua Berko anaumwa malaria, hao wengine sijui, huko waliko wajue wana mkataba na klabu hivyo kama wanaleta mchezo wanakatwa mshahara."