Tigere: Ilikuwa lazima tushinde

KIUNGO mshambuliaji wa Ihefu, Never Tigere aliyehusika na mabao yote mawili yalizoizamisha Yanga juzi kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, amesema ilikuwa lazima washinde mchezo huo kutokana na mtazamo waliojengewa kabla ya kuingia uwanjani na kocha Juma Mwambusi.

Tigere alisema walitambua Yanga ina rekodi ya kutokupoteza mechi 49 na inaongoza msimamo wa ligi, hivyo wakajipanga kuhakikisha wanaitibua na kuandika historia sambamba na kurejea mchezoni.

Ihefu iliivaa Yanga ikiwa mkiani, lakini ushindi huo uliifanya ichupe hadi nafasi ya 13 baada ya mechi 14 na Tigere aliyefunga bao la kwanza kabla ya kuasisti kwa kona iliyofungwa kwa kichwa na beki Lenny Kissu, alisema; “Hakuna kitu kinaumiza kama mnacheza kwa kiwango cha juu halafu hamshindi, ndicho tulichokipitia sisi hadi molari zikawa zinashuka ingawa hatukuwahi kukata tamaa. Kupitia Yanga tumeamka ingawa tumebakiza mechi moja ya duru la kwanza dhidi ya Kagera Sugar tunatamani kushinda.”