Azam kushusha vyuma viwili kutoka DR Congo
Muktasari:
- Wachezaji hao waliwasili alfajiri ya leo wakitokea DR Congo na mara baada ya kutua wanatarajiwa kuingia kwenye hatua za mwisho za mazungumzo kabla ya kusaini mikataba rasmi ya kuitumikia klabu hiyo ya Chamazi.
AZAM FC imewaleta nchini nyota wawili kutoka DR Congo ni beki Jeancy Mpindi Mukuene na winga Henoc Molia kwa lengo la kukamilisha usajili wao kuelekea msimu mpya.
Wachezaji hao waliwasili alfajiri ya leo wakitokea DR Congo na mara baada ya kutua wanatarajiwa kuingia kwenye hatua za mwisho za mazungumzo kabla ya kusaini mikataba rasmi ya kuitumikia klabu hiyo ya Chamazi.
Azam imefanikiwa kushinda vita ya kumshawishi Mpindi anaeichezea Union Maniema ambaye alikuwa akihitajiwa na FC Lupopo ya huko huko Kongo, beki huyo ambaye ameendelea kujijengea jina kutokana na uwezo wake wa kucheza kwa utulivu eneo la nyuma pamoja na uimara wa kuzuia mashambulizi.
Molia kutoka FC Saint-Eloi Lupopo ambaye ni pendekezo ya kocha Florent Ibenge, anatajwa kuwa mchezaji mwenye kasi, uwezo wa kupiga mipira ya mwisho na kucheza nafasi zaidi ya moja kwenye ushambuliaji, kitu ambacho kinaonekana kuvutia benchi la ufundi la Azam linalotaka kuongeza ushindani eneo la mbele.
Kuingia kwa wachezaji hao kunakuja wakati Azam ikiendelea kujenga kikosi chenye uwezo wa kupambana kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa, huku ikionekana kutaka kuwa na mchanganyiko wa uzoefu na nguvu mpya.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa;"Endapo mazungumzo yatakamilika kama ilivyopangwa, Mpindi na Molia watajiunga na orodha ya nyota wapya wanaotarajiwa kuanza safari mpya ndani ya kikosi hicho msimu ujao.
"Kwa sasa hatua iliyobaki ni vipimo vya mwisho, makubaliano ya kimkataba na utambulisho rasmi kabla ya pazia kufungwa kwenye dili hilo la Wakongo hao wawili."
Meneja habari wa klabu hiyo Thabit Zacharia alisema kuwa;"Jambo la muhimu kwa sasa ni kuendelea na mechi zilizosalia, kuhusu masuala ya usajili ni ya uongozi wa juu, mimi kazi yangu ni kumtangaza mchezaji, hivyo sifahamu chochote."