TFF yagawa mipira 100 kuimarisha soka Mwanza

Muktasari:

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa vituo vya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana (Academy) vilivyotolewa na TFF.

Mwanza. Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeombwa kujitanua hadi mikoani kusaka vipaji kuliko kukaa zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam huku likigawa mipira 100 kwa ajili ya kuimarisha soka la vijana mkoani hapa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa vituo vya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana (Academy) vilivyotolewa na TFF.
Mongela amesema kuwa ili kuwa na soka la ushindani lazima TFF itoke Dar es Salaam kuzuru mikoa mingine ikiwamo Mwanza kusaka vijana wenye uwezo.
"Kwanza niwapongeze Tff kwa kuanzisha mpango huu, lakini niwaombe viongozi kutoka ofisini kutembelea mikoa ili kusaka vipaji wasikae sana kwenye mkoa mmoja wa Dar es Salaam," alisema Mongela.
Jumla ya mipira 100 imetolewa kwa Academy 20 ya mkoani humo kwa lengo la kuendeleza michezo nchini.