Tepsie wa Azam moto uleule Stars

Huyo Tepsi ndo kwanza kaanzaa

WINGA machachari wa Azam, Tepsie Evance anayefanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na mabao mawili na asisti moja, ameahidi kuendeleza moto uleule akiwa Taifa Stars inayoshuka uwanjani leo kuvaana na Uganda katika mechi ya kuwania kufuzu Fainali za CHAN 2023.

Tepsie aliyechelewa kuitwa Stars amefunguka kuonyesha ubora wake kwa kiwango cha hali ya juu akiwa katika timu ya taifa.

“Mashabiki kwa jumla wategemee mazuri kutoka kwangu pale tu nitakapopata nafasi ya kucheza na kuipambania nchi yangu kwani wachezaji na benchi la ufundi tumejiandaa vizuri sana kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Tepsie na kuongeza;

“Japo tunaenda kucheza mchezo mgumu na uganda lakini kwa maandalizi tuliyoyafanya kama timu ya taifa ni mazuri sana na niwatake Watanzania kuondoa mashaka juu ya timu hii.”

Akizungumza kuitwa kwake Stars, alisema anajisikia faraja kama kijana mdogo na mwenye ndoto kubwa kwenye soka.

“Najisikia furaha kuitwa kwenye timu ya taifa kwasababu ni ndoto ya kila mchezaji kutumikia nchi yake, kuna vitu vingi vya kujifunza kupitia kaka zangu walionizidi umri na uwezo,” alisema Tepsie.