Tembo Warriors yatinga 16 bora Kombe la Dunia

Tembo Warriors yatinga 16 bora Kombe la Dunia

USHINDI wa Argentina wa mabao 3-2 dhidi ya England jana jioni umeipa timu ya Taifa ya Walemavu ya Tanzania ‘Tembo Warriors’ nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora ya Fainali za Kombe la Dunia nchini Uturuki.

Awali jana asubuhi Tembo waliifunga Uzbekistan mabao 2-0 na kulazimika kusubiri matokeo hayo ya jioni kujua hatma yao. Hiyo Tembo watacheza na Japan kesho Jumatano.

Kocha Msaidizi wa Tembo Warriors, Ivo Mapunda amesema waliwasoma wapinzani wao namna ya kuwakabili ndio maana walishinda mechi yao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ivo alisema; “Tulijifunza kutokana na makosa kwani kama benchi la ufundi ilitupasa kukaa chini na kujua tunaukabili vipi mchezo unaofuata, kwenye uwanja wa mazoezi hatukubadilisha mbinu zetu, kikubwa kilichotusaidia ni namna tulivyowaanda kisaikolojia wachezaji wetu”

“Usiku tulikuwa na kikao kizito kilichoongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Hassan Abbas ambapo tuliwatia moyo wachezaji wetu na kuwaaminisha kuwa wanaweza jambo ambalo limeleta matokeo chanya na kuibuka na ushindi,” alisema Ivo. Nahodha, Juma Kidevu alisema; “Kuna wakati ilitupasa kuongeza nguvu ya kupambana bila kuchoka kutokana na uwepo wa mashabiki nje ya uwanja waliokuwa wakitusapoti kwa kushangilia mwanzo mwisho hivyo hakukuwa na sababu ya kuwaangusha na kuwavunja moyo”

“Uzalendo na kujituma ndizo sababu za kupata ushindi kwenye mchezo uliopita kwani timu pinzani waliokuwa bora na wazoezi kwa kiasi chake lakini sisi hatukuangalia hilo bali kujituma na kuongeza bidiii kila hatua ya dakika.”

Mabao ya Tembo Warriors yalifungwa na Steven Manumbu dakika ya 13, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Alfan Kiyanga ambaye kipindi cha pili dakika ya 38 alipiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja ndani ya wavu licha ya kipa wa Uzbekistan kufanya jitihada za kutaka kuokoa mpira huo.