Tembo Warriors yapata ushindi wa kwanza Kombe la Dunia

Timu ya Taifa ya Watu wenye ulemavu Tembo Warriors, imepata ushindi wa kwanza katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 yanayoendelea nchini Uturuki wakiifunga Uzbekistan mabao 2-0

Ushindi huo mbele ya wababe wa kundi E umewafanya washike nafasi ya pili wakiwa na jumla ya alama nne ndani ya michezo mitatu waliyocheza huku  miwili ya mwanzo wakivuna alama moja baada ya kupata sare ya bila kufungana na Hispania na  wakifungwa mabao 3-0 na Poland.

Mabao mawili ya ushindi ya Tembo Warriors yamefungwa na Steven Manumbu dakika ya 13 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Alfan Kiyanga ambaye na yeye kipindi cha pili mnamo dakika ya 38 alipiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja ndani ya wavu licha ya kipa wa Uzbekistan kufanya jitihada za kutaka kuokoa mpira huo.

Kikosi cha kwanza cha Tembo Warriors kilichoikabili Uzbekistan kiliundwa na golikipa Hassan Ame, Abdulkarimu Khalifa, Shendrack Sembele, Mudrik Azzan, Ramdhani Chomelo, Frank Ngailo pamoja na Alfan Kiyanga.

Hatma ya Tembo Warriors kufuzu hatua inayofuata inategemea na mchezo unaowakutanisha Hispania na Poland mchana wa leo huku kama Hispania akimfunga Poland kwa mabao yasiyozidi mawili basi Tembo Warriors itakuwa imefunzu hatua ya 16 bora.