Tegete ajibu mapigo, Yanga yarudi kileleni

Beki wa Yanga, Shadrack Nsajigwa akipambana na Raphael Kayela wa Ruvu Shooting katika mechi ya ligi kuu Bara kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana, Jumatatu. Yanga ilishinda 1-0
DORIS MALIYAGA, MOROGORO YANGA imerejea kwenye usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting 1-0 kwenye mechi iliyochezwa jana Jumatatu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa. Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 38 na kuwashusha wapinzani wao wa jadi, Simba kwenye nafasi ya pili na pointi zao 37. Shujaa kwa Yanga alikuwa Jerry Tegete, ambaye alizamisha bao hilo dakika ya 77 baada ya kuunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Kiggy Makassy. Tegete, ambaye amefikisha bao la saba kwenye ligi, ameiweka vizuri kisaikoloji Yanga wakati itakapowavaa Simba, Jumamosi wakati ikiwa kileleni. Pamoja na ushindi huo, lakini Yanga ilicheza chini ya kiwango kwani ilishambuliwa vikali na Ruvu Shooting, ambayo ilishindwa kutumia nafasi ilizopata na hasa kipindi cha pili. Yanga ilianza mchezo huo kwa nguvu na Athumani Iddi `Chuji' alipoteza nafasi nzuri dakika ya 22 baada ya kushindwa kufunga akiwa karibu na lango baada ya kupokea pasi maridadi ya Davis Mwape. Revocatus Maliwa wa Ruvu Shootinga alipoteza nafasi nzuri dakika ya 42 kutokana na kupiga shuti lililotoka nje baada ya kutengenezewa mpira na Martine Mlolele. Yanga katika kipindi cha pili ilikuwa na wakati mgumu na kocha Sam Timbe alifikia hatua ya kumtoa mfungaji tegemeo, David Mwape na kumwingiza Iddi Mbaga katika dakika ya 55. Naye kipa wa Yanga Yaw Berko alifanya kazi nzuri ya kuokoa shuti la Mlolele katika dakika ya 64. Yanga itatakiwa kujiweka vizuri kwa pambano dhidi ya wapinzani wao Simba Jumamosi kwani mchezo wa jana ulikuwa ni mgumu kwao na kama Ruvu Shooting ingekuwa makini habari ingekuwa nyingine. Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Sam Timbe alikiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu kwao. "Nimeshukuru kwamba wamepambana tukapata pointi tatu, Ruvu walikamia sana huu mchezo na kitu kingine ni kwamba bado timu inaendelea kuzoea staili yangu ya uchezaji lazima uone baadhi ya kasoro lakini ni katika kuzoea mabadiliko,"alisisitiza Timbe. "Kuhusiana na mechi ya Simba Jumamosi tutaanza kuifanyia kazi kuanzia kesho(leo Jumanne) mazoezini, tunaanda mikakati ya mchezo mmoja baada ya mwingine." Hiyo ni mechi ya tatu ya Timbe ndani ya benchi la ufundi la Yanga tangu asaini mkataba wa wiki 12 kuinoa timu hiyo ya Jangwani. Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Dedebit walipofungwa mabao 2-0 mjini Addis Ababa, kabla ya kuifunga Kagera Sugar bao 1-0. Ruvu Shooting: Mohamed Mbulu, Michael Pius, Oscar Joshua, George Osey, Hamisi Yakuti/Mangasin Mbonosi , Jumanne Juma, Rafael Keyala, Hassan Dilunga, Martine Mlolele, Revocatus Maliwa na Ayoub Kitala. Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephen Mwasika, Chacha Marwa, Nadir Haroub `Cannavaro', Ernest Boakye, Nsa Job, Athumani Iddi `Chuji', Davis Mwape/Iddi Mbaga, Jerry Tegete na Kiggy Makassy.