Tatizo Simba liko hapa

Muktasari:

  • Msimu huu iliondolewa kwa  kuchapwa jumla ya mabao 3-0 na Al Ahly hatua hiyo baada ya kulala 1-0 Kwa Mkapa na kuchapwa 2-0, Cairo International, Misri.

Simba imeondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kwa mara ya nne na mara moja katika Kombe la Shirikisho Afrika ndani ya miaka sita mfululizo.

Msimu huu iliondolewa kwa  kuchapwa jumla ya mabao 3-0 na Al Ahly hatua hiyo baada ya kulala 1-0 Kwa Mkapa na kuchapwa 2-0, Cairo International, Misri.

Hata hivyo, kiuhalisia bado timu hiyo haina matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa inachoombe ni kwa watani zao, Yanga ipoteze michezo ili ikae kileleni na kwa sasa ikiwa na tofauti ya pointi saba, ingwa Simba ina mchezo mmoja mkononi.

Yanga msimu huu hadi sasa imepoteza michezo miwili tofauti na msimu uliopita, huku Simba msimu huu hadi sasa imepoteza mechi mbili. Misimu ya hivi karibuni Simba imekuwa na matatizo mengi hali inayosababisha ishindwe kutamba licha ya usajili mkubwa inaoufanya kila mara kwenye madirisha ya usajili.

Hata hivyo, baadhi ya matatizo hayo yanayoirudisha nyuma klabu hiyo ya mitaa ya Msimbazi, Kariakoo, yamekuwa yakijirudia mara kwa mara  hali inayofanya timu hiyo izidi kudidimia na sasa haina matumani ya kumaliza msimu na kombe lolote, achilia mbali Ngao ya Jamii iliyoitwaa mwanzo wa msimu kwa kuifunga Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

USAJILI TATIZO KUBWA

Linatajwa ndilo tatizo kubwa Simba msimu huu na limeonekana kuigharimu timu hiyo na kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali inayoshiriki.

Simba imekuwa ikifanya usajili ambao haulipi na wachezaji wengi ni wale ambao hawana mikataba kwenye timu walizopita.

Usajili wa washambuliaji wawili, Freddy Michael na Pa Omary Jobe ni kielelezo timu hiyo haipo vizuri kwenye idara ya usajili, kwani walisajiliwa kipindi cha dirisha dogo ili kuisaidia katika michuano ya kimataifa, lakini mwisho wameshindwa hata kupata dakika 45 kwenye kila mchezo.

Michezo miwili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, mastraika hao walijikuta wakipata wastani wa dakika 20 tu kwenye kila mchezo, huku kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha akiwatumia wanaocheza nafasi nyingine kucheza nafasi zao.

Simba iliwaondoa Moses Phiri na Jean Baleka kwenye kikosi na walikuwa wakipata muda mwingi zaidi uwanjani na kuifanya icheze dakika 180 bila kupata bao dhidi ya Al Ahly ikiwa ni mara ya kwanza baada ya timu hizo kukutana mara nane katika historia.

Inaaminika mwisho wa msimu huu, kama siyo wote basi mmoja  kati ya Jobe na Freddy ataondoka na Simba itaingia tena hasara ya kusajili.

UMRI WA WACHEZAJI:

Kwa wastani wachezaji wengi wanaonekana kuwa na umri mkubwa jambo linalosababisha washindwe kwenda na kasi ya soka la kisasa.

Pamoja na kwamba vyanzo mbalimbali vinaonyesha wastani wa umri wa wachezaji wa Simba ni miaka 28, lakini uhalisia unakataa kwa kuwa wengi wenye umri wa chini wamekuwa hawapati nafasi kwenye kikosi hicho na badala wake wanacheza wengi wenye miaka 30 na kuendelea.

Mfano kwenye wastani huo ni  wachezaji kama Ally Salim mwenye miaka 23, Kibu Denis 25,  Ladack Chasambi 20 na Edwin Balua 22 ambao hawana nafasi kubwa kwenye timu hiyo. Kidogo Kibu ndiye anacheza sana.

Kiuhalisia wastani wa umri wa wachezaji wa Simba wanaoanza kwenye mchezo mmoja ni miaka 30, mfano Clatous Chama ana miaka 32, umri uliorekodiwa,  Fabrice Ngoma 27, Saidi Ntibazonkiza 36, Ayoub Lakred 28, Inonga Baka 30 pamoja na Mohammed Hussein 27 na Shomary Kapombe 32.

Kwenye soka la Afrika, asilimia kubwa ya umri uliopo hapo haupo sahihi na mara nyingi itakuwa miaka miwili au mitatu mbele, hivyo timu hii ni ngumu kuhakikisha inapata matokeo bora kila mara kutokana na wachezaji wake wengi kutokuwa na kasi inayotakiwa uwanjani, pia wanaweza kuchoka mapema.

Hii ilionekana kwenye bao la kwanza katika mchezo dhidi ya Al Ahly kwa Mkapa, kutokana na kukosa kasi, wachezaji wanne wa upinzani walifika kwenye boksi la Simba, huku Simba ikiwa nao watatu. Hata bao la kwanza dhidi ya Al Ahly ugenini lilikuwa na mazingira hayo hayo.

MAKOSA YA KIZEMBE:

Simba haikuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa ilizidiwa bali makosa ya wachezaji mmoja mmoja.

Kwenye mchezo wa nyumbani, kosa la Inonga na kushindwa kuuondoa mpira ndiyo liigharimu timu hiyo kulala kwa bao 1-0, mchezo wa pili nchini Misri, kosa la Shomary Kapombe kushindwa kuutoa mpira nje lilisababisha bao la kwanza, lakini bao la pili ni faulo ya kitoto ya Che Malone Fondoh aliyomchezea mchezaji ambaye hakuwa na madhara langoni kwao na kuzaa penalti.

KUFUKUZA MAKOCHA

Simba imekuwa na tatizo la kuondoa makocha kila katikati ya msimu, hii imekuwa ikiifanya timu hiyo irudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Baada ya Simba kulala kwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga, iliachana na kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na kumleta Benchikha.

Hali hii mara nyingi imekuwa ikiizorotesha timu na kumfanya kocha anayekuja kuanza kazi upya mwanzoni mwa msimu na humchukua muda kutengeneza timu upya ndiyo maana hadi sasa, Benchikha hana kikosi cha kwanza cha uhakika.

MAKOCHA WANASEMAJE

Kocha wa Dodoma Jiji, Francis Baraza alisema; “Ukiangalia Simba ambayo imecheza misimu minne hatua ya robo fainali, kuna wachezaji wamecheza misimu yote, hivyo lazima watakuwa na fatiki, wanahitaji kupumzika na kuongezewa nguvu kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi yao.

“Tshabalala kila msimu yupo na anacheza ligi, FA na Ligi ya Mabingwa, hana mchezaji wa kumpa changamoto, hii ni ngumu kwake kucheza kwenye kiwango kikubwa katika kila mchezo bila kuchoka,” alisema.

Kocha wa zamani wa Tanzania Prisons ambaye kwa sasa hana timu, Adolf Rishard, ameliambia Mwanaspoti; “Shida iliyopo ni timu kubwa zinahitaji matokeo ya papo kwa papo, ndio maana wanashindwa kutengeneza timu hata kwa misimu miwili au mitatu mbele ili kujiweka katika nafasi ya kurudisha ushindani wachezaji walionao wamechoka wanatumika sana.”  “Ni ngumu kumtumia mchezaji misimu minne au mitano akakupa kile unachostahili bila kuchoka, pia umri ni shida, unakuwaje na wachezaji ambao wanakata pumzi wakikutana na wapinzani wenye kasi na unategemea kufika mbali.”

ROBERTINHO AWASHA MOTO

Kocha wa zamani wa kikosi hicho kabla ya kurithiwa na Banchikha, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amezungumzia ushindani wa timu hiyo hasa kwenye michuano ya kimataifa na kusema ilipoishia, ilistahili.

Robertinho aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa kwenye Fukwe za Copa Cabana, Brazil timu hiyo ilistahili kuishia hatua hiyo kutokana na aina ya kikosi chao.

Alisema ili timu hiyo ifikie malengo na hata kucheza nusu fainali ya ligi ya mabingwa inahitaji kurudi chini kusaka mastaa wenye kiwango cha kuvaa presha ya Wekundu hao.

Kocha huyo aliyewaachia Simba ubingwa wa Ngao ya Jamii, alisema; “Nikiwa hapo (Simba) nilikuwa nawaambia timu inahitaji muda kurudi kwenye kiwango chake, ndio tulikuwa tunashindana lakini huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kikosi ambacho hakijabalansi.” “Nilishangaa walipokimbilia kuniondoa mimi wakati ukweli unajulikana hata kwa mashabiki, wanaona kuna wachezaji ambao hawakubaliani nao juu ya viwango vyao na sasa watakwenda kwenye usajili wa dirisha kubwa.

“Nadhani wanatakiwa kumeza dawa chungu, kwanza waondoe kundi kubwa la wachezaji wa kawaida, baada ya hapo wakatafute mastaa wenye kiwango cha kuitafutia matokeo, mimi nimekaa Simba, ukiwa kocha pale kila dakika unatakiwa kuwaza unashindaje mechi inayokuja, hili huwezi kufanikisha kama huna watu wa kukupa matokeo.

“Ukimuondoa kwenye timu mchezaji kama Baleke (Jean) unatakiwa kumleta mtu bora kuliko yeye, lakini hili halikufanyika sawasawa, bado wana nafasi ya kurekebisha kama watatulia kwenye usajili, wakatafute wachezaji ambao wataweza kuimudu presha ya Simba lakini sio kama hawa ambao waliokuja sasa.

“Unapokwenda kuwania kucheza dhidi ya timu nne bora Afrika, unatakiwa kuwa na wachezaji ambao watatumia nafasi hizo chache mnazotengeneza, hapa huwezi tena kulaumu mbinu za kocha lazima utazame mara mbili aina ya kikosi ulichonacho.

INONGA, MALONE WABAKI

Akizungumzia uwepo wa taraifa za kuondoka kwa mabeki wawili wa kati, Henock Inonga na Che Malone, Robertinho alisema Simba isithubutu kuwaruhusu mastaa hao kuondoka kwani kazi ya kuunda kikosi kila msimu itawagharimu.

“Ili ujenge nyumba imara unatakiwa kuwa na msingi mzuri, unaona kocha wa sasa amefanikiwa kwa kuwa alikuta kwenye ulinzi kuna mabeki wazuri, watu wanalalamika Kapombe (Shomari), Tshabalala (Mohamed Hussein) wamekwisha, hapana wanahitaji mzunguko mzuri ili wapumzike wametumika sana.

“Wakipata wenzao wazuri wa kushindania nao nafasi kocha atakuwa na wakati mzuri wa kuwaimarisha kwa kuwapa nafasi na kuwapumzisha sawa na Inonga, Che Malone nao wanahitaji beki mmoja wa kati mwenye kiwango ambaye atawapa presha lakini pia kuwapumzisha.

MAKOCHA WAKAZIA

Kocha wa Zesco ya Zambia George Lwandamina ambaye aliangalia mechi mbili za wekundu hao dhidi ya Ahly alisema “Kuna wakati Simba ilikuwa na watu bora sana kule mbele, wakiwa na Chris Mugalu, Bocco (John) na Kagere (Meddie), ilikuwa ukienda kukutana nao lazima ukune kichwa, nadhani wanatakiwa kuumiza kichwa watarudije kutengeneza safu kama ile, kwa sasa hawana watu bora kule mbele.

“Unaona yale makosa mawili waliyofanya Ahly kipindi cha kwanza kipa anapangua na mpira kuwakuta tena wachezaji wa Simba? Ile ilitakiwa moja kati ya nafasi zile iwe goli, kwa kuwa timu kubwa kama Ahly haiwezi kufanya makosa makubwa kama yale kisha yakajirudia.

Naye kocha Julie Chevalier wa Asec Mimosas ya Ivory Coast aliongeza akisema; “Sisi (Asec) ni vile tuliuza wachezaji wetu wengi lakini kama tungekuwa sawa sawa tulitakiwa kuamua mechi zote mbili dhidi yao (Simba), kama wanataka mafanikio zaidi Simba wanatakiwa kuboresha kikosi chao, timu isirudi vile msimu ujao kama wakikutana na timu ngumu itakuwa changamoto kwao.”