Tatizo mtibwa ni hili!
Muktasari:
- Pia alisema katika michezo minne iliyobaki anahitaji japo pointi sita tu ili kujiweka pazuri na kukwepa aibu ya kurudi Championship na kilichobaki kwa sasa ni kila mmoja kushinda mechi zake.
PAMOJA na kukiri ugumu wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Yusuph Chipo ametaja sababu mbili zilizoifanya timu hiyo kuwa katika msoto wa matokeo hadi kupambania kukwepa kushuka daraja.
Pia alisema katika michezo minne iliyobaki anahitaji japo pointi sita tu ili kujiweka pazuri na kukwepa aibu ya kurudi Championship na kilichobaki kwa sasa ni kila mmoja kushinda mechi zake.
Mtibwa Sugar iliyorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kudumu msimu mmoja Championship, haiko pazuri ikiwa nafasi ya 12 kwa pointi 27, pointi ambazo zinaweza kufikiwa na timu zilizopo chini yao.
Katika mechi nne zilizobaki itawafuata Pamba Jiji Juni 17, kisha kurejea nyumbani dhidi ya Simba Juni 24, itaifuata Tanzania Prisons Juni 27 na kumalizia msimu Juni 30 mkoani Lindi kukipiga na Namungo.
Chipo raia wa Kenya, ameliambia Mwanaspoti majeraha ya mara kwa mara kwa baadhi ya mastaa wake na kuhama viwanja iliwapa wakati mgumu katika kucheza mechi zao na kwa sasa kilichobaki ni kukaza na michezo iliyobaki.
Alisema licha ya nafasi waliyopo kuwapa matumaini ya kutoshuka daraja, lakini bado vita ni ngumuna wanasaka japo pointi sita ili kujihakikishia zaidi kuwa salama, akikiri ugumu wa mechi za ugenini.
“Timu nyingi zinashinda nyumbani lakini kwa sasa tunahitaji kupambana kutafuta pointi sita, vijana wako fiti na wanao uwezo wa kufanya vizuri kwakuwa uwanjani wanaonesha kitu,” alisema Chipo.
Kocha huyo aliongeza ligi ya Tanzania imeendelea kuwa imara na bora kutokana na wingi wa wachezaji wa kigeni na Mtibwa Sugar ndio haijawa na nyota wa kimataifa hali inayoongeza ushindani zaidi.