Taswa yapata uongozi mpya, Mwandishi Mwananchi ashinda kwa kishindo

Amir Mhando amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) uchaguzi mkuu uliofanyika leo Februari 5, kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.

Amir amechukua kijiti cha Juma Pinto aliyemaliza muda.

Katika uchaguzi huo, Amir amepata kura 57 na Mbwana Shomari kura 11.

Mwandishi wa habari  za michezo wa Kampuni ya Mwananchi, Imani Makongoro ameshinda kwa kishindo nafasi ya Katibu Mkuu msaidizi kwa kupata kura zote 68 za ndiyo.

Mwandishi wa habari  za michezo wa Kampuni ya Mwananchi, Imani Makongoro ambaye ameshinda kwa kishindo nafasi ya Katibu Mkuu msaidizi kwa kupata kura zote 68 za ndiyo kwenye Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)

Milinde Maona wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) akitangaza matokeo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo,  Halima Bushiri, amesema Imani Makongoro aliyekuwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo amepata kura zote za ndiyo.

"Hakuna kura iliyomkataa, hivyo namtangaza Imani Makongoro kuwa Katibu Mkuu msaidizi wa Taswa," amesema Maona.

Kwenye nafasi ya Katibu Mkuu, Alfred Lucas aliibuka kinara kwa kupata kura  57 na Issa Ndokeji kura tisa huku Michael Noel akikosa kura na mbili zikiharibika.
 
Kwenye nafasi ya mweka hazina, Dina Ismail aliyekuwa mgombea pekee alipata  kura 65 za ndiyo na tatu za hapana.

Kwenye ujumbe Timzoo Kalugila ameibuka kinara kwa kupata kura 62 na Nasongelya Kilyinga kura 60.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu mkuu wa BMT, Neema Msitha, Ofisa michezo wa Baraza hilo, Charles Maguzo ambaye pia ni mlezi wa TASWA aliutaka uongozi huo kutengeneza ushirikiano wa pamoja kwa lengo la kuendeleza Chama.

"Kuwa na ofisi inayotambulika pia ya Chama, najua uwezo huo mnao, Wana Taswa ni watu wa watu hivyo mtashirikiana na wadau wenu kufanikisha hilo na kutoa kadi za uanachama kama kwenye kampeni tumesikia ndani ya miezi mitatu, hivyo wanachama wazipate.

"Kingine ni mabadiliko katiba, yale mnayotaka kwa sasa yawepo, ila Wana habari ndiyo kioo cha jamii mkiandika kwa weledi, hivyo kwenye michezo tuoananishe na matukio mengine nchini kama utalii, viwanda na mengineyo," amesema.

Mwenyekiti wa Taswa, Amir Mhando aliwashukuru wajumbe wote kwa ushirikiano huku akiahidi Chama sasa kinakwenda kuwa cha mfano.

Amir alimshukuru mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Juma Pinto akimuelezea namna alivyojitoa na wakati mwingine kutumia pesa yake ya mfukoni kwa kazi za Chama.

"Wengi walikuwa hawafahamu na mwenyekiti wangu hakuwa mtu wa kujionyesha, lakini tulifanya vitu vingi fungu (bajeti) ikitoka mfukoni mwake," alisema Amir ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti alikuwa Katibu mkuu wa Chama hicho.

Alisema kwa kushirikiana na wajumbe wengine wa kamati ya utendaji, sasa wanakwenda kuifanya Taswa kuwa ya mfano na kuomba ushirikiano wa pamoja na wanachama akisisitiza Taswa ni ya Wana habari wote za michezo.