Tanzania yazidi kuvuna medali Madola

Tanzania yazidi kuvuna medali Madola

Tanzania imejihakikishia medali ya tatu kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola inayoendelea Birmingham, Uingereza.

Ushindi wa RSC wa raundi ya tatu kwa Kassim Mbundwike kwenye robo fainali umeipa uhakika wa medali ya pili ya shaba kati ya tatu ambazo Tanzania  imetwaa msimu huu.

Mbundwike alimchapa Marion Faustino AH Tong kwa RSC baada ya refarii kusimamisha pambano usiku wa kuamkia leo, matokeo yaliyompa fursa Mtanzania huyo kutinga nusu fainali.

Kwa mujibu wa kanuni za ngumi za ridhaa, mabondia wote wanaotinga nusu fainali ni washindi wa medali,  watakaopigwa kwenye hatua hiyo kila mmoja ataondoka na medali ya shaba na washindi watatinga fainali kusaka bingwa na mshindi wa pili.

Kwa matokeo hayo sasa, Mbundwike anakuwa Mtanzania wa pili kushinda medali baada ya Alphonce Simbu kutwaa medali ya fedha kwenye mbio za marathoni na Yusuf Changalawe kujihakikishia pia medali ya shaba mpaka sasa.

Kama watashinda mapambano yao ya wikiendi hii, Changalawe na Mbundwike  watakuwa wametanguliza mguu mmoja kwenye ubingwa, rekodi ambayo mara ya kwanza na ya mwisho ndondi waliiweka kwenye michezo ya 1998.

Michael Yombayomba (sasa ni marehemu) alitwaa dhahabu katika michezo iliyofanyika huko Kuala Lumpur.

Mabondia wengine waliowahi kutwaa medali za fedha na shaba kwenye michezo hiyo ni Titus Simba, Willy Isangula, Bakari Mambea na Haji Matumla.