Tanzania Prisons moto ni uleule

Muktasari:

  • Prisons ilikuwa na moto mkali kwani katika mechi tano za mwisho, ilipoteza moja dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1 huku ikishinda tatu na sare moja na kukaa katika nafasi ya tano kwa alama 28.

WAKATI Tanzania Prisons ikirejea kambini leo Jumatatu, kocha mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally amesema anatarajia kasi yao itakuwa ileile huku akipigia hesabu pointi tatu za KMC ili kusaka nafasi katika nne za juu.

Prisons ilikuwa na moto mkali kwani katika mechi tano za mwisho, ilipoteza moja dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1 huku ikishinda tatu na sare moja na kukaa katika nafasi ya tano kwa alama 28.

Baada ya mapumziko ya takribani siku 14, Prisons inarudi leo kuanza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya KMC utakaopigwa Aprili 12 kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, kabla kusafiri kuwafuata Geita Gold.

Kocha huyo alisema licha ya mapumziko hayo hatarajii kuona mabadiliko yoyote kiufundi kwa vijana wake kutokana na programu alizokuwa amewapa haswa kujifua binafsi.

Alisema wanaporejea mzigoni kazi kubwa ni kujiandaa na mchezo unaowakabili dhidi ya KMC wakihitaji alama tatu ili kujiweka ndani ya nafasi nne za juu kama ilivyo malengo yao.

“Kila mmoja naamini ametumia vyema mapumziko, sitarajii kuanza upya bali kukumbushia na kuendeleza tulipoishia, kila mmoja alipewa programu na matarajio ni kufanya vizuri,”  alisema Ally.

Kocha huyo aliongeza kuwa pamoja na matokeo mazuri waliyonayo lakini hakuridhishwa na ubora wa mabeki kutokana na kuruhusu mabao katika kila mechi akieleza kuwa benchi la ufundi limeona na litaanzia hapo ili michezo iliyobaki wasifanye makosa.

“Tumekuwa tunapata mabao lakini pia tunaruhusu, hili si rafiki sana na tunapaswa kulifanyia kazi kwa michezo hii iliyobaki na tunapoenda mazoezini beki tutaisuka upya,” alisema.