Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania One wa sasa ni nani?

Aishi Manula

Muktasari:

Tanzania ni kati ya nchi za Afrika Mashariki na barani Afrika iliyobarikiwa kuzalisha makipa bora kabisa waliokubalika na kuheshimika kiasi cha kufikia kuteuliwa kwenye kombaini ya timu ya Afrika (All Africa Games) ya mwaka 1973 iliyofanyika Nigeria baada ya Omar Mahadh bin Jabir alipoteuliwa kwenda Mexico.

HAKUNA ubishi kuwa kwa sasa makipa Aishi Manula na Ally Mustafa ‘Barthez’ ndio walio bora nchini. Historia ya soka la Tanzania kabla na baada ya uhuru nafasi ya kipa ndio ilikuwa ya kwanza kabisa kutoa mchezaji wa kulipwa wakati aliyekuwa Tanzania One wa miaka ya 1960-1970 Kitwana Manara ‘Popat’ aliposajiliwa Feisal FC ya Mombasa.

Tanzania ni kati ya nchi za Afrika Mashariki na barani Afrika iliyobarikiwa kuzalisha makipa bora kabisa waliokubalika na kuheshimika kiasi cha kufikia kuteuliwa kwenye kombaini ya timu ya Afrika (All Africa Games) ya mwaka 1973 iliyofanyika Nigeria baada ya Omar Mahadh bin Jabir alipoteuliwa kwenda Mexico.

Kipa huyo wa zamani wa African Sports, Simba na Taifa Stars aliingia kwenye timu hiyo sambamba na mshambuliaji nyota wa zamani, Maulid Dilunga.

Wadau wa soka walio wengi wanaonyesha kuwakubali makipa, Manula na Barthez wanaowika kwa sasa nchini, wakiwataja kuwa ndiyo makipa bora ingawa kiuhalisia wapo makipa wengine hodari wa Ligi Kuu na hata zile za chini kama FDL na SDL.

Kwa mfano wapo kina Deogratius Munishi ‘Dida’, Shaadan Kado, Said Mohammed ‘Nduda’, Manyika Peter Manyika, Benno Kakolanya na wengine wengi ambao kama wataongeza bidii na nidhamu wanaweza kufika mbali zaidi ndani na nje ya nchi.

Kabla sijajikita zaidi kuwajadili Manula na Barthez, ni heshima kuwakumbuka mashujaa wengine walioitumikia nafasi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kuiletea sifa Tanzania nje ya mipaka huku wakijijengea umaarufu mkubwa ndani ya nchi.

Mikoa ya Tanzania zama hizo ikiwa majimbo alikuwepo kipa mashuhuri toka Jimbo la Magharibi (Western Province) huyu ni Abdul Hamid ambaye si rahisi kumsahau kwa waliopata kumuona kipa huyu akilinda lango la Tanzania katika michuano ya Gossage Cup (sasa Kombe la Chalenji) inayochezwa kila mwaka ikijumuisha nchi za Afrika Mashariki na Kati hata michuano ya Sunlight (sasa Taifa Cup).

Zama hizo zilifuatiwa na ujio wa kina Kitwana Manara, kipa wa kwanza kucheza nje ya nchi kabla ya kulihama lango na kugeuka kuwa mshambuliaji matata hasa kwa kutumia kichwa kufunga mabao wakati akichezea Yanga, kombaini ya Dar es salaam na Taifa Stars.

Tanzania iliendelea kuzalisha makipa wengine kama Mbaraka Salum wa Cosmo, Elias Michael wa Yanga aliyejulikana kama Nge Mweusi (Black Scorpion) kutokana na mavazi yake meusi kuanzia soksi hadi jezi na hata unyumbufu wake. Huyu pia aliitendea haki nafasi hiyo katika timu ya Yanga na Taifa Stars, pale Yanga alikuwepo pia Muhidin Fadhili aliyefanya vizuri kama msaidizi wa Elias.

Bado hazina ya makipa bora ilionekana Simba ukianzia na Abdallah Bobea, John Semainda, Greyson Mwamwaja na Hassan Mlapakolo hadi alipoibuka kipa mashuhuri kuliko wote huyu ni Athumani Mambosasa.

Mambosasa anatajwa kama kipa bora zaidi katika historia ya Tanzania, kipa huyu aliyekuwa na kimo kirefu, unyumbufu, wepesi pia mahesabu akiwa langoni ataendelea kukumbukwa na wengi hususan Simba akiwa kichocheo kilichoisaidia timu hiyo kuweka historia iliyotukuka katika anga za kimataifa.

Anakumbukwa kwa tukio la mwaka 1974 Simba ikiikabili Mehala El Kubra pale Misri kwa mchezo wa nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika, ambapo akiwanyima Waarabu mabao ya wazi kabisa na ndipo walipoamua kumponda kwa mawe wakati mpira ukiendelea. Kama hiyo haikutosha akavuliwa ‘glovsi’ zake kwa imani za kishirikina wakidhani zilikuwa na nguvu za giza ndani yake, pamoja na vitimbi vingine vingi tu vikilenga kumfanya apoteze umakini.

Tanzania iliendelea kama kawaida kuwatoa makipa wengine wengi zaidi kama vile Katembo kutoka Zanzibar mmoja wa makipa wazuri akicheza wakati mmoja na nguli wa walinda mlango katika historia ya soka nchini, Mahadhi, kabla ya zama za kina Hemed Mussa wa Tanga wakifuatiwa na kina Ally Bushiri na Rifaat Said wa Zanzibar mnamo miaka ya 90 sambamba na na Steven Nemes pia Sahau kambi.

Ebu nitoe nafasi maalumu kwake, Juma Pondamali mmoja wa makipa walioiwezesha Tanzania kufuzu kucheza fainali za Afcon 1980, huyu jamaa alikuwa na historia ya aina yake, mcheshi wakati wote wa mchezo, mtundu, mjanja na alisifika sana kwa kucheza na saikolojia ya washambuliaji wa timu pinzani.

Miongoni mwa utundu wake uliotaka kumponza akiwa na timu ya taifa ni pale alipoudaka mpira vizuri kisha kumrudishia mpira mshambuliaji wa timu pinzani akashindwa kufunga sababu hakuamini kama ni kweli kipa anaweza kufanya vile.

Haya sasa sikiliza hawa nao waliofuatia na kutawala soka la ndani ya nchi akiwemo Mohamed Mwameja kipa aliyejiunga Simba akitokea Coastal union ya Tanga baada ya kuchezea timu ya Ndovu ya Arusha. Mwameja ndie aliyekomaza jina Tanzania One, aliyelirithi kutoka kwa Idd Pazi ‘Father’.

Mwameka alifanya mambo makubwa akiwa klabu ya Simba na Taifa Stars, miongoni mwa kumbukumbu ambazo ni vigumu kusahaulika ni pale alipoiwezesha Simba kucheza fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993 dhidi ya Stella Abdijan ya Ivory Coast. Baadaye upande wa Yanga akaibuka Sahau Kambi aliyerithi jina hilo.

Huyu ndiye kipa pekee wa Yanga aliyeweza kupewa jina la Tanzania One baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa kina Joseph Fungo na Hamis Kinye.

Kuondoka kwa Mwameja na kina Steven Nemes na Peter Manyika wa Yanga ndiko kulikotoa nafasi kwa Juma Kaseja kurithi mikoba na kutawala nafasi hiyo ndani ya Simba na Taifa stars. Huyu jamaa bado yuko katika fani akimalizia kipindi chake cha zaidi ya mwongo mmoja langoni.

Huyu jamaa naye historia yake imejipambanua kwa mengi mema aliyoutendea mchezo huu wakati mwingine unapata shida kuamini nani alitoa mchango mkubwa kwa vizazi vya hivi karibuni kati ya Mwameja na Kaseja.

Kazi aliyoifanya Kaseja kuiwezesha Simba kuvunja mwiko na kuitoa Zamalek mashindanoni ni historia ya aina yake katika soka la Tanzania hasa unapokumbuka kuwa kila timu zetu zinapokutana na zile za Misri sisi wenyewe hujitanguliza kibla tayari kwa kuchinjwa.

Baada ya utangulizi huo sasa tujikite moja kwa moja kuwaangalia makipa wetu Manula na Barthez, wote wakiwa katika ubora wao lakini bado hakuna hata mmoja kati yao tumesikia kwa dhati akirithi jina la Tanzania One hii inatokana na nini?

Manula ni kipa mzuri kimo chake ni cha wastani analinda lango lake vizuri na hadi sasa amefungwa mabao 16 katika Ligi Kuu. Manula ana tatizo la mawasiliano kati yake na mabeki wake kazi ambayo ndiye anapaswa kuifanya akiwa mtu wa mwisho hilo lilijionyesha wazi katika mechi ya marudiano na timu ya Bidvest Wits, pale Chamazi na limeonekana tena katika mechi ya Azam dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Hata hivyo, Manula alifanya kazi ya ziada kuwazuia Waarabu hao kutoka na ushindi mnono katika mechi ile na siku zote msaada wake husaidia Azam kushinda mechi zake.

Huyu ndiye kipa chaguo la kwanza la kocha Stewart Hall wa Azam na Boniface Mkwasa wa Taifa Stars.

Manula anayo nafasi ya kufika mbali na kurithi ufalme wa watangulizi wake ana tatizo la kujiamini kupita kiasi hatimaye kupoteza umakini.

Kwa upande mwingine Barthez ni mtulivu sana langoni, anapanga vizuri mabeki wake na anao uwezo mkubwa wa kukabiliana na adui mmoja (one against one) lakini ana udhaifu mkubwa katika kucheza krosi labda inatokana na kimo chake kifupi kama ilivyojionyesha mechi ya kwanza kati ya Tanzania na Algeria Dar na mechi ya Yanga na APR pale Kigali.

Barthez amefungwa mabao 12 katika Ligi Kuu kabla ya mechi ya Mwadui, kwa hali hiyo bado yeyote kati ya hawa atakayeongeza bidii na kujiwekea malengo anaweza kurithi jina la Tanzania One, ingawa wadau bado wanasita kumtamka mrithi wa jina hilo labda hawajamuona bado.

Barthez pamoja na kucheza vizuri katika mechi ya Yanga na El Ahly mwishoni mwa wiki alirudia kosa la kutowapanga mabeki wake jambo lililosababisha timu yake kufungwa bao rahisi na El Ahly ambalo limeiweka Yanga katika hali ngumu.

Haya wewe msomaji una maoni gani katika hili ebu tuambie ni nani Tanzania One kati ya wawili hawa Aishi Manula na Ally Mustapha ‘Barthez’.

NB:Kwa swali la wiki iliyopita- Shomari Kapombe wa Azam na Juma Abdul wa Yanga. Sms zilizotumwa ni 357. Matokeo Abdul alipata 185 sawa na asilimia 52, huku Kapombe akipata 164 sawa na asilimia 46. Waliosema wote wazuri walikuwa nane sawa na asilimia mbili. Jibu 0784-611005.