Tambwe anawalamba

STRAIKA wa zamani aliyeacha alama kubwa ndani ya Simba na Yanga, Amissi Tambwe anajiandaa kudaka mpunga wake kutoka kwa mabosi wa Jangwani ili kutenguliwa kwa adhabu waliyopewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) la kutosajili kwa vipindi vitatu mfululizo.

Tambwe analamba fedha hizo baada ya kuishtaki Yanga Fifa kutokana na kumzungusha kumlipa malimbikizo ya fedha zake za usajili na mishahara tangu amtema misimu miwili iliyopita, l straika huyo Mrundi amesimulia kila kitu alipopokea simu ya kutafuta muafaka na mabasi wake wa zamani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe anayeichezea Polisi ya Djibouti alisema amepokea simu ya Makamu Mwenyekiti wa Usajiliwa Yanga na mmoja wa wakurugenzi wa GSM, Injinia Hersi Said akimtaka kuwasiliana na mwanasheria wake na kuweka sawa taarifa kamili ya deni lake na kuiwasilisha kwao.

“Nilipokea simu ya yule bosi Hersi ameniambia niwasiliane na mwanasheria wangu na tuweke taarifa za deni langu sawa na kisha tumtumie haraka yeye,” alisema Tambwe na kuongeza;

“Tayari tumeshafanya hivyo na amenishukuru kwa kufanya hivyo na kwamba wanalifanyia kazi suala hilo kwa haraka,naona ni hatua nzuri acha tuone watamaliza lini.”

Aidha Tambwe alisema hakuwa na nia ya kufikia hatua ya kuishtaki Yanga lakini usikivu mdogo wa baadhi ya viongozi wa klabu hiyo ndio iliyoababisha wafike hapo.

Mfungaji Bora huyo mara mbili katika Ligi Kuu Bara akiwa na Simba na Yanga, alisema viongozi wa Yanga ni lazima wawe makini na kesi kama hizo hasa zinapofika Fifa ambao hawataki kuona mambo ya kupoteza haki ya mtu.

“Hili halikuwa suala la kufika hapa kati yangu na Yanga, hii ni klabu ambayo naiheshimu sana na mashabiki wake lakini shida kuna baadhi ya viongozi pale ipo siku watasababisha matatizo makubwa kwa klabu hii,” alisema Tambwe aliyefunga jumla ya mabao 75 katika misimu sita akiwa nchini.

“Wanachukulia vitu hivi kama masihara leo kesi hii ipo kwangu ambaye naiheshimu Yanga lakini inaweza kutokea kwa mtu ambaye akaamua kufanya ukatili watakuja kufungiwa vibaya kwa suala dogo tu la kushindwa kuwa na mawasiliano mazuri,” alisema mkali huyo na kuongeza;

“Yapo mengi yalinitokea tangu nilipoachana na Yanga ambayo hayakunifurahisha lakini niliamua kunyamaza na kuyamaliza mwenyewe,nilifurahi nilipopokea simu ya Hersi tumeongea vuzuri na naamini tutalimaliza hili kwa haraka ili nipate haki yangu na Yanga iendelee na maisha yake.”

MSIKIE SENZO

Naye bosi wa ushauri wa uongozi wa Yanga Senzo Mazingisa alilithibitishia Mwanaspoti kwamba madai ya namna hiyo yapo mengi na Yanga inayamaliza taratibu na kwamba hata mada ya Tambwe yatamalizwa wiki ijayo.

“Sababu kubwa ya uongozi wa klabu na GSM kusimamia mchakato huu wa mabadiliko ni kutaka kuona klabu inandoka katika eneo kama hili,hii kesi itamalizwa wiki ijayo mapema hakuna shida,” alisema Senzo.