Tabora United yamtimua kocha Goran

Muktasari:
- Goran alijiunga na Tabora United Agosti mwaka jana kama kocha mkuu kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuwa umalizike mwishoni mwa msimu huu kabla ya kufikia uamuzi wa kuvunjwa mapema leo hii.
BAADA ya sintofahamu ya muda mrefu hatimaye kocha Goran Kopunovic wa Tabora United ameingia kwenye orodha ya makocha waliotemeshewa vibarua vyao katika klabu za Ligi Kuu Bara msimu huu, akiwa ni kocha wa 14 kupigwa chini hadi sasa.
Kocha huo wa zamani kwa muda mrefu alikuwa akihusishwa kutaka kutimka klabuni hapo kutokana na kilichoelezwa kushindwa kusikilizwa matakwa yake na viongozi, lakini mapema jana jioni uongozi wa klabu hiyo uliweka bayana kuachana na kocha huyo kwa makubaliano ya pande mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa klabu hiyo iliyotolewa na kusainiwa na Ofisa Habari, Christina Mwagala, ni kwamba kocha huyo aliyeajiriwa katikati ya mwaka wamekubaliana kwa pande zote mbili kusitishiwa mkataba kuanzia leo Machi 21.
Katika taarifa hiyo, inaeleza Tabora imefikia uamuzi huo kutokana na kutorodhishwa na mwenendo wa matokeo ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
Goran alitua Tabora kama kocha mkuu kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuwa umalizike mwishoni mwa msimu huu na hadi anaondoka ameiongoza timu hiyio kucheza 21 ikishinda minne, sare tisa na kupoteza minane, ikifunga jumla ya mabao 15 na kufungwa 25 ikishika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 21 kama ilizonazo Mashujaa iliyopo juu yake na Geita Gold inayoshika nafasi ya 14 zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Goran anaingia kwenye orodha ya makocha waliotimuliwa na timu zao kabla ya mwisho wa msimu, akiwamo Habib Kondo aliyekuwa wa kwanza kusitishwa mkataba na Mtibwa Sugar.
Pia wamo Roberto Oliveira Robertinho (Simba), Zubeir Katwila na Moses Basena (Ihefu), Mecky Maxime (Kagera Sugar), Mwinyi Zahera (Coastal Union), Cedric Kaze (Namungo), Hemed Morocco (Geita Gold), Ernst Middendorp, Ricardo Ferreira na Thabo Senong (Singida Fountain Gate), Fred Felix 'Minziro' (Tanzania Prisons) na Melis Medo.
Ni klabu za Yanga, Mashujaa, JKT Tanzania, KMC na Azam FC ndizo pekee kwa msimu huu hazijabadilisha makocha walioanza nao msimu huu.