Straika aibwaga Yanga atimkia Ulaya

Mshambuliaji aliyekuwa akiwindwa na Yanga, Sankara Karamoko amekamilisha uhamisho wa kutua katika Klabu ya Wolfsberger AC ya Austria baada ya kudumu ndani ya Asec Mimosas kwa miaka mitano.

Karamoko (20), ambaye alijiunga na Asec mwaka 2019 akianzia timu ya vijana amekamilisha uhamisho huo baada ya timu hiyo kukubaliana na Wolfsberger AC inayoshiriki Ligi Kuu Astria maarufu kama Ausrian Bundesliga.

Katika msimu huu akiwa na Asec, Karamoko amefanikiwa kuwa kinara wa mabao kwa timu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akikofunga mabao manne.

Wolfsberger AC iko katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi nchini humo ambapo Asec imeeleza kwamba mshambuliaji huyo ameuzwa kwa dau lisiloweza kuwekwa wazi.

Karamoko anakwenda kuungana na mshambuliaji mwenzake wa zamani wa Asec, Karim Konate ambaye naye aliuzwa msimu uliopita kwa klabu ya Redbull Salzburg.

Tayari mshambuliaji huyo ameondoka nchini Ivory Coast akielekea  Ausrtia kukamilisha dili hilo ambapo endapo atafuzu vipimo vya afya atasaini mkataba utakaomfanya aishi huo hadi 2027.

Yanga iliweka mitego yake ili kumnasa mchezaji huyo wakati wa dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, lakini ilishindikana katika ishu ya makubaliano kwa kilichodaiwa kwamba timu yake ilikuwa na mpango wa kumuuza Ulaya.