Stars yapewa mwamuzi wa kadi

Kikosi cha timu ya Taifa kesho kinashuka dimbani kutupa karata yake ya kwanza katika mchezo wa kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Niger mchezo utakaochezwa saa 1:00 usiku nchini Morocco kwenye uwanja wa Stade de Marrakech.

Katika mchezo huo wa kundi E ambao ni wa kwanza, Stars licha ya kwamba itakuwa na kibarua kigumu ndani ya uwanja dhidi ya Niger, mtihani mwingine ni mchezo huo kuamuliwa na refa, Bekouassa Lotfi (36) raia wa Algeria.

Lotfi ameonyesha kuwa refa ambaye hana utani hata kidogo anapokuwa ndani ya uwanja kwani suala la kutoa kadi kwa wachezaji ni jambo la kawaida.

Refa huyo katika mechi 10 za mwisho kuchezesha ametoa kadi za njano 62 na kadi nyekundu tatu hivyo ni wazi mastaa wa Stars inabidi wawe makini katika dakika 90 za mchezo huo ili wasiweze kudhurika kwenye mechi zijazo.

Lotfi katika mechi moja ya US Monastiri dhidi ya Etoile du Sahel alitoa kadi 10 za njano na moja nyekundu, hiyo ndio rekodi yake kubwa katika kugawa kadi kwenye mchezo mmoja.

Upande wa kadi chache ambazo anatoa katika mchezo mmoja ni sio chini ya kadi tatu, alitoa kwenye mechi ya US Biskra dhidi ya CS Constatine na El Bayadh dhidi ya CS Constatine.