Stars yapaa Ethiopia kutesti uzi mpya

Muktasari:
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mart Nooij, alitangaza kikosi cha wachezaji hao kwa ajili ya kambi hiyo ya wiki moja kabla ya kuvaana na Mafarao wa Misri Juni 14, kwenye Uwanja wa Borg el Arab, mjini Alexandria huko Misri.
KIKOSI cha wachezaji 23 kilitarajiwa kupaa jioni ya jana Alhamisi kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kuweka kambi ya kujiandaa na pambano la kuwani kufuzu Fainali za Afrika (Afcon-2017) dhidi ya Misri, wakitarajiwa kuanza kutumia uzi wao mpya uliozinduliwa juzi.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mart Nooij, alitangaza kikosi cha wachezaji hao kwa ajili ya kambi hiyo ya wiki moja kabla ya kuvaana na Mafarao wa Misri Juni 14, kwenye Uwanja wa Borg el Arab, mjini Alexandria huko Misri.
Wachezaji walioondoka ni Makipa; Deogratias Munishi, Aishi Manula na Mwadini Ali.
Mabeki ni Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Aggrey Morris, Mwinyi Haji, Salum Mbonde na Juma Abdul. Viungo ni Mwinyi Kazimoto, Abdi Banda, Salum Telela, Frank Domayo, Jonas Mkude na Said Ndemla wakati washambuliaji ni Simon Msuva, John Bocco, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Mrisho Ngasa na Juma Liuzio.
Aidha kikosi kingine cha Stars kitaondoka kesho Jumamosi kwenda Rwanda kucheza mechi ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.