Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stars yaendeleza unyonge kwa Kenya

Muktasari:

Kenya ilikuwa bingwa mtetezi wa mashindano ya Chalenji baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2017 pindi mashindano hayo yalipoandaliwa nchini mwao.

TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars imemaliza katika nafasi ya nne baada ya kupoteza mchezo wake wa kuwania mshindi wa tatu wa mashindano ya Chalenji dhidi ya Kenya kwa mabao 2-1.
Mchezo huo ambao ulichezwa katika Uwanja wa KCCA uliopo Lugogo, Kampala kuanzia saa 7.00 mchana, ulionekana kupooza huku timu hizo zikigawana vipindi katika umiliki wa mpira.
Kipindi cha kwanza kilitawaliwa zaidi na Kenya ambao mbali na kuwa na muunganiko mzuri wa kitimu, walikuwa na haraka ya kufanya maamuzi pindi waliponasa mpira na kutumia vyema makosa ya wachezaji wa Stars kuwaadhibu.
Haikushangaza kuona Kenya wakienda mapumziko huku wakiwa wanaongoza kwa ushindi wa mabao 2-0 ambayo yalipachikwa na Kenneth Muguna na Abdallah Hassan katika dakika za 16 na ile ya 36.
Mbali na kufunga mabao hayo mawili, Kenya walipoteza nafasi kadhaa ambazo ikiwa wangekuwa makini kuzitumia vizuri, wangeweza kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa idadi kubwa ya mabao.
Mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi la Kili Stars chini ya Kocha Juma Mgunda kwa kuwatoa Eliuter Mpepo na Jonas Mkude na kuwaingiza Paul Nonga na Baraka Majogoro yalionekana kuiongezea uhai na kutawala kipindi cha pili kwa kuwalazimisha Kenya kurudi nyuma kujilinda na kutengeneza nafasi ambazo zilianza kuonyesha mwanga wa kusawazisha mabao hayo.
Stars ilijaribu kulazimisha kupenya kuingia langoni mwa Kenya mara kwa mara katika kipindi hicho cha pili lakini kikwazo kilionekana ni ukuta wa Kenya uliiongozwa na nahodha Joash Onyango ambao ulikuwa makini kuwadhibiti Stars.
Kiungo Baraka Majogoro alifanikiwa kuilinda vyema safu ya ulinzi ya Stars na kuiunganisha vyema timu kutokana na pasi zake zilizofikia walengwa kwa usahihi jambo lililoipa uhai timu.
Kwa upande wa Nonga, aliongeza nguvu kwa Ditram Nchimbi ambaye katika kipindi cha kwanza alitengwa na kutopata msaada wa kutosha wa kukabiliana na safu ya ulinzi ya Kenya jambo lililofanya mabeki wa kati wa timu pinzani kucheza kwa uhuru mkubwa.
Uwepo wa Nonga uliwalazimisha mabeki wa Kenya kubaki nyuma na kutosogea mbele mara kwa mara kusaidia kuanzisha na kutengeneza mashambulizi.
Hilo lilipelekea Stars kupata bao pekee la kufutia machozi katika dakika ya 83 kupitia kwa Gadiel Michael aliyefunga kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Omar Abdulkadir kutoka Somalia, baada ya beki Joash Onyango kunawa mpira katika eneo lake la hatari wakati alipokuwa akijaribu kuokoa krosi ya Hassan Dilunga.
Kabla ya kupiga krosi hiyo, Dilunga alifanya kazi ya ziada kumtoka beki wa pembeni wa Kenya, Samuel Olwande na kumimina majalo kutokea upande wa kushoto na ndipo Onyango alipounawa mpira na kuamriwa kuwa pigo la penati.
Mara baada ya kuingia kwa bao hilo, Kilimanjaro Stars ilijitahidi kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Kenya lakini safu ya ulinzi ya wapinzani ilikuwa makini kuondosha hatari hizo.
Katika harakati za kulinda ushindi, Kenya walifanya mabadiliko kwa kuwatoa Moses Mudavadi na Abdallah Hassan huku nafasi zao zikichukuliwa na Daniel Sakari na Ayoub Masika.
Beki wa Stars, Kelvin Yondani na kiungo Jonas Mkude walionyeshwa kadi za manjano katika kipindi cha pili kutokana na faulo walizocheza kwa wachezaji wa Kenya, Samuel Olwande na Oscar Wamalwa.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, kocha wa Stars, Juma Mgunda alisema kuwa wapinzani wao walistahili kupata ushindi.
"Mpira ni mchezo wa kutumia nafasi. Wenzetu walitengeneza nafasi wakazitumia vizuri na mwisho wa siku wakaweza kulinda ushindi wao lakini niwapongeze wachezaji wangu pia kwa kupambana ingawa mwisho wa siku tulishindwa kutumia nafasi ambazo tulitengeneza.
Kiujumla mashindano haya yamekuwa na umuhimu mkubwa kwetu kwa sababu tulikuja na vijana kadhaa ambao ndio kwanza wanaanza kuichezea timu ya Taifa hivyo kucheza mechi tano za kimataifa kama hizi," ni uzoefu wa kutosha ambao wameupata.
Kocha wa Kenya, Francis Kimanzi alitoa pongezi kwa vijana wake kwa kuibuka na ushindi huku akilalamikia ratiba ya mashindano hayo.
"Namshukuru Mungu kwamba tumemaliza mashindano tukiwa hatuna wachezaji waliopata majeraha makubwa hivyo wanarejea katika klabu zao wakiwa wazima.
Hata hivyo ratiba sio rafiki na inawaumiza wachezaji kwani hawapati muda wa kutosha wa kupumzika na miili yao inachoka jambo ambalo lina athari kwa afya zao na kuwaweka katika uwezekano wa kupata majeraha," alisema Kimanzi