SPOTI DOKTA: Siku ya Afya Duniani, mwanamichezo zingatia haya

Muktasari:

  • Kauli mbiu hiyo ndio imeifanya kona ya Spoti Dokta kuja na ujumbe huu kwa maelfu ya wanamichezo na mashabiki wanaopenda michezo kama ajira, burudani na kama nyenzo ya kukabiliana na magonjwa.

Keshokutwa ni siku ya Afya Duniani chini ya mwamvuli wa Shirika la Afya (WHO) kwani Aprili 7 ya kila mwaka ni siku ya kimataifa ya afya. Mwaka huu kaulimbiu inasema “Afya yako, haki yako.”


Kauli mbiu hiyo ndio imeifanya kona ya Spoti Dokta kuja na ujumbe huu kwa maelfu ya wanamichezo na mashabiki wanaopenda michezo kama ajira, burudani na kama nyenzo ya kukabiliana na magonjwa.


Siku hii ya kimataifa itaadhimishwa kwa kampeni mbalimbali zinazohusu afya ikiwamo kutolewa kwa elimu ya afya kujikinga na magonjwa au matatizo ya afya ambayo ni mzigo kwa jamii.


Kwa mujibu wa ujumbe wa WHO unasema kuwa duniani kote haki ya afya ya mamilioni ya watu inazidi kutishiwa. Inaelezwa kuwa magonjwa na majanga yanakuwa sababu za vifo na ulemavu.


Wanamichezo na mashabiki ambao wanatazama michezo wote wanaweza kupata magonjwa au kupata majanga yanayoweza kuwafanya wawe wagonjwa au kupata ulemavu.


Wanamichezo wakiwa katika majukumu yao wanakutana na majeraha yatokanayo na michezo ambayo machache sana huwa tishio kwa afya au kupata ulemavu.


Matatizo ya afya yanayotokea katika michezo si mzigo wa afya ya jamii kiasi cha kutishia kuifungia michezo, ukilinganisha na matatizo ya afya makubwa kama vile kifua kikuu, Ukimwi na malaria.


Ila ni muhimu kujua kuwa afya yako ni haki yako, iwe ni mchezaji au mtazamaji afya yako ni mtaji wako. Mchezaji akiwa hana afya njema ina maana hataweza kucheza.


Wakati shabiki au mtazamaji asipokuwa na afya njema ina maana hataweza kufika katika burudani ya michezo au atashindwa kufanya mazoezi mepesi kwa ajili ya kujenga afya yake.


Moja ya mambo ambayo yanaweza kusababisha afya yako kuwa shakani ni pamoja jamii kuhusika na mambo ya uchafuzi wa hali ya hewa au uharibifu wa mazingira


Lakini kama mchezaji na mashabiki hawashikamani na njia za kujikinga na magonjwa maana yake ni kuwa na wao wanatishia kuharibu afya zao na wengine. Wanayofanya yanawanyima kuwa na haki ya afya njema.


Kwa mchezaji ambaye anafanya maisha kama sehemu yake ya ajira anapaswa kufahamu kuwa kupewa huduma na klabu yake ni haki yake.


Ndio maana wanapopata majeraha klabu na timu za taifa huwa zinawajibika kuhakikisha wanapata huduma muhimu za afya.
Klabu zinatambua kuwa haki ni afya kwa watu wote ikiwamo wachezaji wanaowaajiri. Ina maana kuwa huduma za afya anatakiwa kupata popote anapokuwepo.


Huduma nyingi za msingi ambazo ni haki ya mchezaji ni pamoja na kupata maji yaliyo safi na salama, kuishi katika mazingira safi na salama, kula vyakula vyenye lishe bora, mazingira ya kufanyia mazoezi na kucheza yaliyo salama na kulala na kupumzika katika mazingira mazuri.


Katika nchi zetu tunazoishi tayari huwa na huduma za afya za msingi ambazo serikali kama Tanzania ambayo Katiba yake inatambua kuwa afya ni moja ya haki za msingi kwa wananchi wake.


Lakini changamoto zipo ambazo kila siku zinajitokeza ikiwamo uchafuzi na uharibu wa mazingira, uunguzaji wa mafuta na ukosefu wa huduma za uhakika za afya kwa baadhi ya maeneo.


Afya ni haki ya msingi ya binadamu, tunaposema afya maana yake ni kuwa mkamilifu kimwili, kiakili na kijamii pasipo uwepo wa ugonjwa wowote.


Maelfu ya wanamichezo duniani wamekuwa na mchango mkubwa katika jamii ikiwamo kuburudisha, kutoa ajira, kuchangia maendeleo na sehemu ya kujenga jamii yenye afya bora kwani michezo ni afya.


Lakini na wao ni sehemu ya jamii ambayo wanapaswa kujua kuwa afya zao ni haki yao. Kutowajibika kwake, kutowajibika kwa klabu yake na kwa nchi anayoishi ni tishio kwa haki ya afya yake.


Haki ya afya ina maana kuwa kila mtu anapaswa kuwa na haki ya kudhibiti afya na mwili wake mwenyewe ikiwamo kufanya hatua zote za kujikinga na magonjwa na kupata huduma mapema anapoumwa.


Ukiwa kama mwanamichezo au mshabiki unapaswa moja kwa moja kuwa mfano wakuigwa wakushikamana na njia za kujikinga na magonjwa, kuwa kinara wa kutunza mazingira unayoishi pamoja na kutochafua au kuharibu vyanzo vya maji.


Kwa wale wanamichezo ambao tayari wanamafanikio makubwa ni muhimu kuwa mabalozi wa afya kwa kuionyesha jamii umuhimu wa kuwa na afya njema kwa kufanya mazoezi mepesi kama nyenzo mojawapo ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.


Ikumbukwe pia mchezaji atastaafu soka na kuna maisha baada ya soka. Hivyo ni vyema kuishi katika mazingira au nchi ambayo si tishio kwa yale mambo ambayo yananyima haki ya afya yako kuwa bora.

JANABI AZINGATIWE
Nikiwageukia wale watazamaji michezo ambao wanakuja viwanjani kupata burudani, napenda kuwakumbusha kwamba na wao wanatakiwa kuchukua hatua kubwa dhidi ya afya zao.


Siku za karibu Profesa Mohamed Janabi, mburugenzi mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili amekuwa akizungumza sana katika vyombo vya habari na huku pia katika makundi ya mitandao ya kijamii. Anayoyasema usichukulie ni utani ni kweli na unapatswa kuyazingatia kwa ajili ya afya yako.


Kuna viashiria vyote kuwa magonjwa ya kuambukiza yanaendelea kushika kasi na kuwapata watu ikiwamo ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la juu la damu, magonjwa ya mishipa ya moyo, kisukari, kiharusi na ugonjwa sugu wa figo.


Profesa Janabi ambaye pia ni mdau mkubwa wa soka mara kwa mara amekuwa akihamasisha jamii kuchukua hatua za mapema za kujikinga na maradhi hayo.


Anaeleza namna gharama za matibabu kwa anayeugua magonjwa yasiyoambukiza kuwa ni mzigo kwa serikali na mgonjwa. Hatua za kujikinga za mapema ndizo nyenzo ya msingi kuepukana na mzigo huo.


Pia anaeleza kuchukua hatua katika ulaji holela wa vyakula ikiwamo kupunguza kiwango cha sukari, vyakula vya wanga na mafuta hasa yatokanayo na wanyama.


Vilevile anahimiza kufanya mazoezi mepesi ikiwamo kuhakikisha unatembea angalau hatua 10,000 kwa siku au kufanya mazoezi mepesi kama utembeaji wa haraka ama ukimbiaji wa kawaida kidogokidogo.


Kwa mujibu wa WHO mazoezi mepesi yanatakiwa kufanyika kwa dakika 150 kwa wiki. Ni sawa na kufanya dakika 30 kwa siku katika siku tano za wiki.


Hata kwa wanamichezo kuna wakati wataastaafu na umri nao utakwenda. Watahitajika kufanya mazoezi mepesi kama njia ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Muhimu kuepuka pia matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Chukua hii
Afya yako ni mtaji wako. kujinga ni rahisi kuliko kujitibu. Shikamana na ushauri wa madaktari.