Song afichua fedha ilivyomng'oa Arsenal
Muktasari:
Song alijiunga na Arsenal mwaka 2006 na akaichezea michezo 205 kisha mwaka akajiunga na Barcelona ambako alitwaa taji moja la Ligi Kuu Hispania 'La Liga' na Supercopa de Espana.
London, England. Kiungo wa zamani wa Arsenal, Alex Song ameweka wazi kuwa hakufikiria mara mbili kufanya maamuzi ya kuondoka Arsenal na kwenda Barcelona baada ya kutangaziwa mshahara mnono.
Raia huyo wa Cameroon alitimka Arsenal na kwenda Barcelona kwa ada ya uhamisho wa Pauni 15 milion msimu wa joto wa 2012.
Hatua ya kwenda Hispania kulimfanya kiungo huyo kati kupata ongezeko la mshahara kutoka Pauni 55,000 alizokuwa akilipwa kwa wiki ndani ya Arsenal hadi Pauni 70,000.
Song (32) ameeleza kuwa uamuzi aliochukua miaka nane iliyopita haukuwa mgumu kutokana na nguvu ya fedha.
'Nilikutana na mkurugenzi wa michezo wa Barcelona na akaniambia sitopata nafasi ya kucheza michezo mingi,
Nilijua kuwa sasa nitakuwa milionea, sikuyapa nafasi aliyokuwa akiyasema Mkurugenzi. Wakati Barcelona ilinipa mkataba, na nikaona ni pesa nyingi , sikufikiria mara mbili.
"Ninasema kila wakati, kijana wa miaka 20 ambaye anaendesha Ferrari maisha yake ni duni kwa sababu haujafanya chochote bado. Lakini mtu wa miaka 50 ambaye anaendesha gari la maana 'Bentley', ni mtu wa kumheshimu." alisema
Song pia ameelezea jinsi alivyopigwa na butwaa pindi ambapo alipoliona gari la Thierry Henry alipofika mazoezi.
"Nilipofika Arsenal, nilienda mazoezini kisha nikaona mfalme akifika (Thierry Henry) akiwa na gari lakini adhimu, gari lilikuwa la thamani mno.Nilijiambia kuwa ninahitaji gari ile ile kwa gharama yoyote.
Niliporudi siku nyingine mazoezini akaniuliza gari yako iko wapi nilimweleza kuwa haiendani na hadhi yangu. Niliachana nayo kwa sababu niliona inanimalizia mafuta bure." alisema Song.