Solskjaer asingizia mipira, mwenzake ashangaa

Muktasari:

Lakini, Solskjaer amedai mipira inayotumika kwenye michuano hiyo Molten haikuwa mizuri kwa wachezaji wake hasa ukizingatia kwamba kulikuwa na mvua na upepo wa baridi kwenye mchezo huo dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Ubelgiji.

MANCHESTER, ENGLAND . KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema mipira ya hovyo ndicho kitu kilichoifanya timu yake kushindwa kuichapa Club Brugge na kuambulia sare ya 1-1 kwenye Europa League juzi Alhamisi usiku, shukrani kwa bao la kusawazisha la Anthony Martial.
Bao la kipindi cha kwanza la Martial liliwapa Man United faida ya kufunga ugenini katika michuano hiyo ya mtoano ambapo kwa ipo kwenye hatua ya 32 bora na wiki ijayo kitapigwa kipute cha marudiano uwanjani Old Trafford.
Lakini, Solskjaer amedai mipira inayotumika kwenye michuano hiyo Molten haikuwa mizuri kwa wachezaji wake hasa ukizingatia kwamba kulikuwa na mvua na upepo wa baridi kwenye mchezo huo dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Ubelgiji.
“Ilikuwa mechi ngumu dhidi ya timu iliyojipanga vyema na kwenye mazingira magumu,” alisema Solskjaer.
“Sidhani kama ilikuwa moja ya mechi nzuri, tuliboronga sana na hali ya hewa pia, uwanja na mipira ziliongeza ugumu zaidi. Mipira ilikuwa tofauti na ilikuwa migumu kuichezea, lakini ilikuwa hivyo kwa timu zote. Mepesi sana, chukueni mmoja mjaribu.
“Tumepata sare ya kufunga, hivyo watapaswa kufunga na wao watakapokuja Old Trafford, na kama watataka sare basi ni lazima iwe zaidi ya bao moja.”
Kocha wa Bruges, Philippe Clement alisema: “Tumepata mipira hii kutoka UEFA, sio ya kweli. Kwenye Europa League mechi zote zinatumia mipira ya aina moja, hivyo sidhani kama kuna tatizo kwenye hilo.”
Bruges walipata bao la kuongoza dakika ya 15 tu baada ya makosa yaliyofanywa na kipa wa Man United, Sergio Romero kutoka golini na kumruhusu Dennis kufunga kirahisi, lakini Martial alisawazisha katika dakika 36 na hivyo kufikisha mabao yake 14 msimu huu.
Kocha Clement amelalamika kwamba kipa Romero alipaswa kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na rafu aliyomchezea Dennis.