Skauti Simba azungumzia ishu ya Mayele

SIMBA ilipolala bao 1-0 dhidi ya bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly, mmoja wa watu waliokuwa jukwaa kuu ni skauti mkuu wa kusaka vipaji wa wekundu hao, Mels Daalder.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mels amezungumza mambo mbalimbali ikiwamo suala la usajili kwa Wekundu wa Msimbazi, lakini alipoulizwa kuhusu straika wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele juu ya kujiunga na Simba hakuwa na jibu la moja kwa moja, lakini akagusia ugumu uliopo katika dili la mkali wa aina hiyo.

“Kupata mchezaji bora sio kitu rahisi kama ambavyo wengi wanadhani hasa unapoingia sokoni kutafuta mshambuliaji wa kati, mfano angalia Yanga baada ya kuondoka Mayele (Fiston) alikuwa mchezaji mzuri kwao alipoondoka akaletwa Konkoni (Hafiz) kumbuka alitoka ligi ya Ghana akiwa amefanya vizuri sana. lakini alipofika hapa akashindwa kuwa na muendelezo mzuri na sasa wamemuondoa.

“Washambuliaji bora ni wachache sana, unaweza kumpata unayemuona bora ukakuta kuja nchi kama Tanzania anaona shida anataka kwenda Ulaya kwahiyo sio Simba pekee inasumbuka na hili, angalia Al Ahly ililazimika kwenda Borussia Dortmund kununua mshambuliaji Anthony Modeste kwa fedha nyingi, hii unaweza kupata picha ya ugumu wa kupata washambuliaji wazuri ulivyo

Raia huyo wa Uholanzi anakaribia kufikisha mwaka mmoja sasa kwenye ajira hiyo kubwa yenye maslahi mapana ya Simba katika ishu za kuwa na kikosi cha wachezaji mastaa na wenye vipaji, matamanio ambayo mashabiki na wanachama wengi wa wekundu hao walikuwa wakitarajia.

Baada ya mchezo huo mashabiki wa Simba wamekuwa wakilalamika juu ya ubora wa wachezaji wao hususan kwenye safu ya ushambuliaji huku wakidai kwamba haina mwendelezo mzuri wa kiwango uwanjani.


USAJILI MASTAA WAPYA SIMBA

Mels anaeleza juu ya kuhusika kwake katika usajili wa mastaa wapya waliosainiwa dirisha dogo la usajili akisema: “Kusema ukweli nimehusika katika karibu sajili zote kwa namna moja au nyingine, nilihusika kwenye tathmini ya wachezaji hawa lakini kuhusu uamuzi wa mwisho hilo kawaida ni suala la uongozi wa klabu.

“Kazi yangu ni kutafuta wachezaji au kama wao wanaona wamepata mchezaji watanitumia na tutashauriana kwa kutazama taarifa zake za kiufundi na hata umri lakini pia huwa naandaa listi ya wachezaji ambao nawaona au kuongea na mawakala wenye wachezaji mbalimbali kulingana na mahitaji ya timu, hivi ndivyo tunavyofanya haya majukumu kwasasa.”


IKITOKEA SIMBA IMEMKATAA MCHEZAJI

“Ukiwa kama skauti una kazi pia ya kuangalia uwezo wa klabu kifedha, ni vigumu kuwaletea Simba mchezaji anayecheza kikosi cha kwanza kwenye klabu kama Mamelodi au Ahly kisha nikawaambia huyu anafaa tumsajili, najaribu kuhakikisha tunapata wachezaji sahihi kwa uwezo wa klabu kulipa, Simba inaweza kuchukua mchezaji anayetoka ligi ya Senegal, Zambia, Congo na kadhalika.


JOBE NA FREDY WAMEFELI SIMBA?

“Hapana ni mapema kusema wamefeli, ukiangalia mchezaji kama Fredy (Kouablan) ni mshambuliaji ambaye amefanya kitu kikubwa kwenye ligi ya Zambia mpaka Simba inamchukua akifunga mabao tisa, tukumbuke Zambia ligi yao iko vizuri kama utailinganisha na Tanzania kwa ujumla ingawa miaka ya karibuni Tanzania inaonekana kuja juu kwa kasi kushinda Zambia.

“Unajua washambuliaji wakati mwingine ili wafanye vizuri ni namna gani unawapa nafasi ya kujiamini. Unapokuja kwenye timu mpya kila kitu kinakuwa kipya kwako, kwa wachezaji ambao kwa mara ya kwanza wanajiunga na timu kubwa yenye presha ya matokeo kama Simba inakuwa sio rahisi kufanya kile kinachohitajika kwa haraka.

“Nadhani watu hapa wanatakiwa kuelewa kitu, usajili wa mchezaji ni ‘risk’, sio kwamba kila ukimchukua mchezaji anayefanya vizuri eneo analotoka basi atakuja kwako ataendelea na kasi ile, hii ipo duniani kote, unachofanya unafuatilia rekodi zake mbalimbali kwa kuangalia mechi zake nzima anavyocheza lakini pia kuna vile vipande vya ubora wake akiwa uwanjani.

“Baada ya hapo unaangalia pia alikuwa anacheza mechi zipi ngumu na matokeo yake anafanya kipi kwenye hizo mechi sasa unaweza kukuta hayo yote mchezaji anakuridhisha na bado anaweza kuja kwako na akashindwa kuonyesha ubora ambao mliutarajia, wapo wachezaji ambao pia wanachelewa kuzoea mazingira lakini baadaye wakishajipata wanafanya makubwa, unahitajika uvumilivu kiasi.”

STAILI MPYA SKAUTI MUBASHARA

“Kwasasa nimekueleza namna tunavyofanya kazi lakini sasa nadhani Simba inatakiwa kwenda hatua nyingine bora ili kupunguza makosa kwa kufanya skauti ya mubashara yaani unasikia kuna mchezaji bora sehemu fulani unaangalia mikanda yake unavutiwa na unamfuata mpaka huko aliko unamuona kwa macho yako anacheza sawasawa na vile ambavyo umeona mikanda yake baada ya hapo unafanya uamuzi, hii ndio njia bora ambayo hapa Simba bado hatujaanza kuitumia sana ambayo klabu nyingi zenye nguvu kubwa ya fedha zinafanya.”


TATIZO FEDHA PIA

Mashabiki wengi wa Simba wanatamani kuona klabu yao ikisajili mastaa wa maana wanaong’aa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hata Kombe la Shirikisho, hapa Mels anaeleza changamoto iliyopo: ”Simba inafuatilia hayo yote kupitia kazi yangu, wapo wachezaji ambao tumeshawachukua kutoka kwenye mashindano hayo lakini wengine wale bora zaidi.

“Mfano kumchukua mchezaji anayecheza kikosi cha kwanza cha Petro Atletico, Mamelodi unahitaji bajeti kubwa nadhani changamoto kubwa iko hapo, huyo mchezaji unayemuona kwanza analipwa fedha nyingi na yupo ndani ya mkataba, klabu yake itahitaji fedha nyingi, labda usubiri mpaka mkataba wake umalizike hapo unaweza kufanya kitu unaangalia hali ya klabu yako unakwenda kufanya uamuzi kwa maeneo ambayo unaona utayamudu.”


CHANGAMOTO YA MAJUKUMU YAKE

“Kufanya kazi hii sio rahisi na wala sijaanzia kufanya majukumu haya hapa Simba, nilikuwa kwenye dawati la skauti pale FC Twente ya Uholazi pale mambo mengi yalikuwa yakifanyika kisasa zaidi unafuatilia takwimu mbalimbali za mchezaji na mikanda yake ya video iliyochambuliwa kisasa baada ya hapo mnamfuatilia kwa kwenda kumuona moja kwa moja uwanjani akicheza baadaye mnafanya uamuzi.

“Hapa Simba ni tofauti, kwanza unaweza kukuta sehemu mchezaji mzuri na hana hata hiyo mikanda ya mechi alizocheza wala ligi yao haionyeshwi na hapo bado hamuwezi kumfuata moja kwa moja mpaka huko anakocheza, ndio maana nasema Simba sasa inatakiwa kuanza angalau njia hii kuweza kujiridhisha juu ya ubora wa wachezaji inaowataka.”


ALIIONAJE MECHI YA AHLY

“Ilikuwa mechi nzuri lakini kitu muhimu kuliko vyote kwenye soka ni kufunga mabao, Ahly pia kipa wao (Mostafa Shobeir) ni kipa mzuri, alikuwa na mechi nzuri, aliokoa mashambulizi mengi kama lile la Che Malone (Fondoh), Saido (Said Ntibazonkiza) na kipindi cha pili akafanya kazi nyingine nzuri kuzuia shuti la Luis (Miquissone) ni kipa mzuri, tulitakiwa kutumia zile nafasi kupata mabao.

“Nadhani bado hatujamaliza kama tutacheza kama tulivyocheza Ijumaa nyumbani tunaweza kushinda kule ugenini, tunatakiwa kwenda kule na kufanya kitu tofauti, kama ukipata bao la kutangulia na la mapema inaweza kuwa mechi nzuri kwa Simba kule Cairo.

“Nadhani pale tuliposhindwa kufunga mabao, kwenye soka hata kama wewe ni winga au kiungo mshambuliaji unapopata nafasi unatakiwa kutulia na kuitumia, jambo la wachezaji wapya ambao tuliwaleta kushindwa kuwa na tija kwa haraka nadhani pia iliigharimu timu, ilikuwa lazima tuwalete wachezaji hawa wawili baada ya Baleke kutakiwa kuondoka kutokana na ofa kubwa iliyoletwa mezani ambayo Simba hawakuwa na kauli kubwa kwa vile mchezaji alikuwa hapa kwa mkopo, lakini pia kuondoka kwa Phiri (Mosses). Bahati mbaya walioingia hawakuwa na kasi ya kuzoea kwa haraka ukizingatia waliingia kupitia usajili wa dirisha dogo.

“Usajili wa dirisha dogo kawaida sio rahisi sana kupata wachezaji wale bora ambao mnawataka na unajua kuondoka kwa Baleke ilikuwa lazima ile dili ifanyike, Mazembe walipokea ofa kubwa ya kutoka Libya ambayo kama Simba wangesema haondoki basi mwisho wa msimu angeondoka bila klabu kupata kitu kwahiyo soka pia ni biashara ili Simba ipate pesa ilitakiwa ikubali biashara ile ifanyike wakati ule ili Mazembe wapate chao na Simba ambao walimpa nafasi nao wapate chao.

“Kuhusu Phiri nadhani ilikuwa inaonekana alikuwa hapati muda wa kutosha wa kucheza na hili alikuwa hafurahii na njia nzuri ilikuwa kumpa changamoto mpya atoke kwa mkopo kupata nafasi ya kucheza kule Power Dynamos.