Prime
Skauti Simba amkataa Dube usajili mpya
Muktasari:
- Miongoni mwao ni washambuliaji hatari watatu wenye ubora wa kujua kufunga na anaamini kama klabu ikipata fungu la kuwang’oa huko walipo watakuwa na msaada mkubwa kwa Simba na watabadili stori kabisa msimu ujao.
TUNAENDELEA na mahojiano na skauti mkuu wa Simba, Mel Daalder na hapa anafunguka mambo mbalimbali yanayohusu usajili wa Wekundu hao, lakini akiweka wazi kwamba tayari kuna mashine tano ameshaziwasilisha kwa mabosi wa klabu hiyo huku akisisitiza kwamba Prince Dube aliyeikacha Azam bado si aina ya wachezaji anaodhani watapindua matokeo Msimbazi.
Simba ilitajwa kuwania saini ya washambuliaji Prince Dube wa Azam na ikapeleka ofa iliyokataliwa kwa madai kwa haikukidhi viwango lakini za ndaani kabisa hata staa huyo walishindwa kumfikia kwani tayari inadaiwa yuko chini ya himaya ya Yanga ambayo bado haijapeleka ofa rasmi.
“Namfahamu Dube ni mshambuliaji bora anajua kufunga lakini unajua amecheza hapa kila mtu anajua juu ya ubora wake siwezi kusema kama yupo kwenye listi ya wachezaji ambao Simba wanawataka. “Hivyo pia kwa Fiston Mayele alikuwa na wakati mzuri sana alipokuwa hapa na Yanga ni mshambuliaji mzuri mwenye kiwango bora lakini bado yuko kwenye klabu yake mpya ya Pyramids sitaweza kuzungumzia lolote lakini unapokuwa unahitaji mchezaji kuna mambo mengi ya kuangalia muendelezo wa kiwango chake bora.
“Unaweza kuangalia pia rekodi yake ya kuwa na majeraha kuna mambo mengi unatakiwa kuyapima wakati unataka kufanya maamuzi ya kumchukua au kumfuata mchezaji kwa ajili ya kumsajili kwenye timu yako, kwa klabu za Afrika wangetamani kuwa na mchezaji kama Dube au Mayele akiwa kwenye kiwango kama alivyokuwa pale Yanga.
“Nafahamu Simba inahitaji wachezaji bora lakini kwa Dube bado hajapata muda wa kutosha kuonyesha kiwango chake kwenye mashindano ya Afrika Zaidi ya kucheza sana ligi ya hapa ndani Simba ikijipanga itaweza kupata washambuliaji bora zaidi Afrika hii bahati mbaya tulifanya maamuzi wakati ambao hatukufanya kazi na kupata watu bora kulingana na uhitaji wa wakati ule.”
“Majibu mengi ya maboresho ya kikosi chetu cha Simba yapo tayari, bahati nzuri changamoto za kikosi chetu sasa zimeonekana mapema, dirisha dogo sio rahisi kupata watu bora sana na hili ndilo lililotughalimu baada ya wachezaji waliopo kutakiwa kuondoka kwa lazima,” anasema skauti huyo.
“Mpaka sasa tayari wachezaji bora ambao tutawasajili dirisha kubwa wapo tayari. Tulishafanya kazi ya kuwatafuta ambao wakija hapa tunaamini watabadilisha hali ya kikosi chetu kuwa bora.
“Hii imekuwa rahisi kwa kuwa tunaelekea mwisho wa msimu wachezaji wengi mikataba yao inafikia tamati. Pia timu nyingi zinaweza kukubali hata kuuza kwa kuwa wanaamini watapata wachezaji wengine bora kwa kuwa muda wanao wa kutafuta wengine kuliko wakati wa dirisha dogo.
“Tuna majina matano ya wachezaji bora ambao tumewapata imebaki hatua ndogo ya kumalizia mazungumzo nao ambalo hili litafanywa na viongozi wa juu wa klabu katika hao watano - watatu ni washambuliaji - wao wataamua kuwachukua wote au wangapi kulingana na bajeti na nafasi.
“Hawa wapo ambao wanacheza sasa mashindano ya Afrika ya klabu na wengine walicheza haya mashindano na wengine ni vijana ambao wanaweza kuichezea Simba kwa muda mrefu.
“Wapo pia wachezaji wa ndani ambao tayari tumeshawapata ambao nao watajumuishwa kwenye hiyo listi tayari kwa kwenda kufanyiwa uchaguzi wa mwisho na viongozi na makocha.
“Hawa wa ndani wapo ambao wanatoka klabu kubwa na wengine klabu zingine kama Geita Gold, Singida, Ihefu, Coastal Union na zingine naamini wachezaji hawa wataleta nguvu mpya ambayo mashabiki wa Simba wataifurahia.
“Huwa nakuja hapa Tanzania mara tatu kwa mwaka kufuatilia mechi za Ligi ya Mabingwa ambazo Simba inazicheza nakumbuka mara ya mwisho nilikwenda Morocco tulipokuwa tunacheza kule na baadaye Uganda.
“Lakini pia hata kutafuta wachezaji wa ndani wazuri pia ni jukumu langu nafuatilia mechi za hapa kwa video au wakati mwingine kama hivi nimekuja nitakwenda kwenye mechi mbali mbali kuangalia wachezaji sahihi kwa ajili ya Simba.
“Kama nilivyosema kabla kwamba kufanya kazi ya kumfuatilia mchezaji moja kwa moja uwanjani kwa kwenda uwanjani hii ni bora zaidi naamini Simba itaifanyia kazi.
“Inakupa nafasi nzuri ya kujua tabia za mchezaji akiwa uwanjani, mfano utaona ana mchango gani kwa timu wakati timu yake ina mpira na haina mpira, hili huwezi kuliona sana wakati unaangalia video zake.
ANAWEZAJE PEKE YAKE?
“Sio rahisi kufanya majukumu haya peke yako, wachezaji wako wengi kutoka mataifa tofauti lakini naelewa kwamba mwanzo una changamoto zake, kwanza lazima tuipongeze Simba kwa kuanza hatua hii ambayo huko nyuma haikuwepo.
“Ninafanya kazi kwa ushirikiano na maskauti wenzangu kutoka mataifa mengine ambao wanafika kwenye mataifa kama Senegal na kwingine tunashirikiana kupeana taraifa mbalimbali za wachezaji bora.
“Nafanya hii kazi peke yangu hapa Simba ingawa hata viongozi nao wanaweza kuwaona wachezaji bora wataniletea listi yao na kisha nitawafuatilia na baadaye wanakwenda kufanya maamuzi ya mwisho .
USAJILI SIMBA UNAFANYIKAJE
“Kwanza unaanzia kwa makocha ambao wataleta mapendekezo yao baadaye watayaleta kwenye kikao cha pamoja na viongozi tutajadili kwa pamoja
“Kama kuna wachezaji ambao tulishawaona kulingana na mahitaji yaliyo mezani kutoka kwa makocha tunawapa wanaangalia na kuona wapi tunaweza kuanza kuzungumza nao ambalo hilo sasa ni eneo la uongozi huko nawaachia wao.
SIMBA INAWAHITAJI HAWA
“Ukiangalia kikosi chetu cha sasa unaona wazi kwamba bado kuna uhitaji wa watu bora wa eneo la mwisho la ushambuliaji, kama timu inatengeneza nafasi na hazitumiki kutokana na ubora wa wachezaji hapo unatakiwa moja kwa moja kutafuta watu ambao ni bora kwa kutumia nafasi, tupo kazini kutafuta watu hao bora wakati huu ambao makocha nao wakipambana kuwaongezea ubora hawa waliopo sasa.
“Unajua kwenye kufunga hatuwezi kuwaangalia namba tisa pekee balio hata kama unacheza winga au kiungo mshambuliaji unatakiwa kufunga na hili ndio lililotugharimu kwenye mechi ya Al Ahly, tukubaliane kwamba Ahly ni timu kubwa lakini ikifanya makosa nadhani ilistahili kuadhibiwa, huwezi kupata nafasi nyingi kwenye mechi kubwa kama ile.
MAWASILIANO YAKE NA BENCHIKHA
“Ukiwa skauti lazima uwe na mawasiliano na kocha mkuu, huwa tunawasiliana na makocha hata sasa nazungumza sana na Benchikha (Abdelhak), ukiacha kazi yangu ya uskauti ambayo huwa tunaongelea kuhusu wachezaji pia nina cheti cha taaluma ya uchambuzi wa kimbinu wa timu pinzani.
“Huko nyuma wakati tunacheza na Al Ahly, Wydad Athletic na hata Al Ahly nimewahi kufanya kazi ya kusaidia ushauri kwa kuzichambua hizo timu zinavyocheza na Simba kisha nawapa makocha kwa kuwapa taarifa za ubora wa wapinzani,mapungufu yao,wanakabaje,wanapigaje mipira iliyokufa.
PRESHA YAKE NA SIMBA IKO HAPA
“Presha ipo unajua Simba ni klabu kubwa lazima kila msimu iwanie mataji yote inayoshiriki kwa ukubwa wake hata mimi skauti wa klabu pia natakiwa kutimiza wajibu wangu inavyotakiwa kufikia malengo ya klabu, presha nyingine huwa naipata kwenye mechi kama Simba ikipoteza kama mchezo wa Al Ahly.
“Nakumbuka tulipopoteza dhidi ya Wydad kwenye dakika za mwisho niliugua kwa siku kadhaa unajua ukiacha hii kazi pia naipenda Simba kwa miaka sita sasa nilichagua kuifuatilia hii klabu, natamani kuiona siku moja ikishinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.”
MO ANACHOTAKA KUTOKA KWAKE
“Huwa sina hulka ya kuongea na MO (Mohamed Dewji) ingawa ni mtu anayetamani kuona Simba inabadilika maono ambayo hata bodi ya Simba inawaza hivyomara kwa mara kutekeleza majukumu yangu muda mwingi huwa naongea na mwenyekiti wa bodi na hata ofisa mtendaji mkuu hao ndio watu ambao nawasiliana nao mara kwa mara katika majukumu yangu, ripoti zangu zote naziwasilisha kwa viongozi hao.”
SIMBA NA UBINGWA WA AFRIKA
“Naiona Simba inaweza kuja kuchukua taji la Afrika muda si mrefu, kwasasa haipo mbali kufikia huko siku itafanikiwa kuvuka kwenda kucheza nusu fainali baada ya hivi karibuni kuishia sana hapa kwenye robo, ukiangalia hata mpira ambao tulicheza na Al Ahly.
“Utaona kwamba hatuko mbali sana, kinachotakiwa ni kukiboresha kikosi chetu ili kiwe na afya bora Zaidi ya kucheza hatua hizo mbili za juu.
“Kuna aina ya wachezaji ambao tunatakiwa kuwaongeza ambao watatufikisha huko, kuna ubora ambao upo kwenye timu kama Petro Atletico, Mamelodi Sundowns ambao kwa Simba inatakiwa kufikia hapo, hizo ni timu ambazo zilifanya vizuri msimu uliopita na sasa bado ziko vizuri kitu muhimu ni kuendelea kuijengea uimara wa kushindana na timu hizi kubwa.
“Kupata hao wachezaji inahitajika bajeti nzuri naamini huko tunakokwenda viongozi wanaona hali ya soko la kupata wachezaji bora lilivyo wataweza kuimarisha uchumi wa klabu na kupata wale wachezaji wakubwa na wenye viwango bora unajua soka pia ni fedha. Tupe maoni yako kuhusiana na habari hii; 0658-376 417
Inaendelea kesho.