Singida BS yashusha bosi mpya

Muktasari:

  • Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Sikwane amepewa cheo hicho kikubwa ndani ya timu hiyo na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa rasmi kama Mtendaji Mkuu wao mpya.

KLABU ya Singida Big Stars imefikia makubaliano ya kumuajiri Ofisa Mtendaji Mkuu mpya, Olebile Sikwane raia wa Botswana kuanzia msimu ujao wa mashindano mbalimbali ya Ligi Kuu Bara na yale ya Kimataifa.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Sikwane amepewa cheo hicho kikubwa ndani ya timu hiyo na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa rasmi kama Mtendaji Mkuu wao mpya.

"Taarifa hizo ni za kweli lakini muda ukifika watatangaza wenyewe rasmi, ni mtu mwenye utaalamu mkubwa na Soka Barani Afrika na Duniani hivyo tuna imani naye kubwa," kilisema chanzo chetu.

Akizungumza na Mwanaspoti Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ibrahim Mirambo alisema hajua taarifa hizo ingawa kama kutakuwa na jambo lolote jipya kuhusu wao basi idara yao ya habari itaujulisha umma.

"Hilo suala mimi silijui kwa sababu ndio kwanza nalisikia kutoka kwako, kuhusu mambo yetu yote ya klabu huwa tunatoa taarifa rasmi hivyo niseme wazi kwa sasa hakuna kitu kama hicho," alisema.

Licha ya kauli hiyo ila Mwanaspoti linatambua Sikwane amepewa cheo hicho akichukua nafasi ya John Kadutu aliyekuwa akikaimu kutoka kwa Dismas Ten aliyepigwa chini tangu Januari mwaka huu.

Sikwane amewahi kufanya kazi katika timu ya Gaborone United ya nchini kwao kama Meneja Mkuu huku pia akihudumu kwenye Chama cha Soka Botswana (BFA) akiwa kama Mkuu wa Operesheni na Mashindano.

Mbali na kuhudumu katika nafasi hizo ila Sikwane anatambuliwa na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) kama wakala wa wachezaji.