Singida Black Stars yaanza na kipa wa Afcon

Muktasari:

  • Kipa huyo ambaye alikuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika alikosaini Horoya mwanzoni mwa 2022, anatarajiwa kuanza kutumika kuanzia msimu unaokuja.

Timu ya Singida Black Stars imekamilisha usajili wa kipa raia wa Sierra Leone, Mohamed Kamara (24) akitokea Horoya AC ya Guinea kwa mkataba wa miaka miwili atakayeanza kutumika kikosini hapo kuanzia msimu ujao.

Kipa huyo ambaye alikuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika alikosaini Horoya mwanzoni mwa 2022, anatarajiwa kuanza kutumika kuanzia msimu unaokuja.

Inaelezwa kuwa Singida ina uhaba eneo la makipa, hivyo usajili wake utakwenda kuongeza ushindani kwa makipa Fikirini Bakar,  Khomen Abubakar na Haroun Mandanda ambao wapo kikosini.

Kamara ambaye ana uzoefu na mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Afcon alikocheza 2021 na anakumbukwa katika mechi mojawapo ya mashindano hayo aliisaidia Sierra Leone kuokoa mkwaju wa penalti dhidi ya Algeria.

Baada ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo aliibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mechi kwa kuokoa baadhi ya hatari langoni kwake pamoja na penalti.

Akizungumzia ishu ya kipa huyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Peter Andrew amesema bado hawajapokea ripoti ya kocha juu ya kuongeza kipa mwingine, hivyo hizo ni tetesi.

"Sisi wenyewe tumeona taarifa hizo mtandaoni. Nafikiri tusubiri msimu uishe ndio tutajua juu ya ripoti ya kocha lakini kwa sasa hizo ni stori tu tuna makipa watatu," amesema Andrew.