Simba yaua, Yanga mdebwedo

Kiungo ya Yanga, Haruna Niyonzima kushoto akiwania mpira na beki wa JKT Ruvu, Damas Makwaya wakati wa mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. JKT Ruvu ilishinda 1-0. Picha na Juma Mtanda.
Michael Momburi, Arusha na Juma Mtanda, Morogoro MABINGWA wa Ngao ya Jamii, Simba wameendeleza makali yao kwa kuichapa JKT Oljoro 2-0 katika mchezo ulioshuhudia kadi nyekundu mbili, huku mabingwa watetezi Yanga wakipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Simba ikicheza kwa kujiamini kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ilipata mabao yake mawili kupitia kwa Emmanuel Okwi na Patrick Mafisango wakitumia nafasi zilizotegenezwa na Felix Sunzu. Kocha Moses Basena alipata faraja ya kumtumia mshambuliaji wake, Gervais Kago kwa dakika 20 za mwisho mchezaji huyo akichukua nafasi ya Haruna Moshi, kabla ya kushuhudia Sunzu akipewa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro kwa kumpiga kiwiko Othman Omary dakika 90. Wakati Simba ikisogea kileleni mwa ligi mapema, watani zao Yanga wameendelea kupata machungu baada ya kupokea kipigo cha pili ndani ya wiki moja walipokubali kuchapwa kwa bao 1-0 na JKT Ruvu, goli lililofungwa kwa penalti na Kessi Mapande. Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mshambuliaji Okwi aliipatia Simba bao la kuongoza katika dakika ya 3 kwa shuti kali lililomshinda kipa Shahibu Issa wa Oljoro baada ya kupokea pasi ya Sunzu. Kiungo Mafisango aliwainua mashabiki wa Simba kwa mara ya pili kwa kutumia uzembe wa mabeki wa Oljoro walioshindwa kuokoa mpira wa kichwa wa Sunzu na kufunga bao la pili katika dakika 13. Kutokana na hali ya kiwanja cha Sheikh Amri Abeid kuwa siyo nzuri wachezaji wa timu zote walicheza soka ya kubutua muda wote, lakini mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba walitumia vizuri udhaifu na uoga wa kipa wa Oljoro kupiga mashuti ya mbali na kupata mabao yao kwa haraka. Oljoro waliamka na kufanya mashambulizi yao kupitia Roshua Rashid na Sunday Paul, lakini walikosa mbinu za kuwapenya Victor Costa na Juma Nyoso. Ngome ya maafande hao ilikuwa na kazi kubwa ya kuwakabili Sunzu, Okwi na Haruna walioonekana kuelewana zaidi kwenye mchezo huo na kupitisha pasi fupifupi. Uzoefu wa ligi ulioneka kuwa ndio kikwazo kikubwa kwa Oljoro inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Oljoro walirudi kipindi cha pili wakiwa wamebadilika na kujiamini zaidi huku wakitembeza viatu kwa washambuliaji wa Simba, hadi pale beki wao Omary Juma alipotolewa kwa kadi mbili za njano na nyekundu kwa kitendo chake cha kumpiga kibao Amir Maftah katika dakika ya 81. Morogoro; Mabingwa watetezi Yanga wakiwa kwenye uwanja wa Jamhuri, waliingia uwanjani wakiwa bado na mawazo ya kupoteza Ngao ya Jamii hali iliyomfanya kocha Sam Timbe kubadilisha wachezaji 7, walionza dhidi ya Simba siku ya Jumatano usiku. JKT Ruvu ikicheza soka ya kujiamini, kutulia na kutawala vizuri sehemu ya kiungo ilifanikiwa kupata bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Kessi Mapande na kumwacha kipa Saidi Mohamed asijue la kufanya. Mwamuzi Oden Mbaga aliamuru penalti hiyo baada ya beki wa Yanga, Bakari Mbegu aliyechukua nafasi ya Nadir Haroub kumwangusha kwenye eneo la hatari Hussein Bunu. Katika mchezo huo viungo wa Yanga, Nurdin Bakari, Rashid Gumbo, Julius Mrope na Haruna Niyonzima walishindwa kupitisha mipira kwa washambuliaji wao huku wakionekana kukosa msaada kwenye ulinzi pia. Wakati wa mapumziko mabingwa mara 22, Yanga walitoa kali pale walipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa dakika mbili na kurudi uwanjani ambako kocha wao Timbe alikaa nao na kutoa mawaidha yake uwanjani kinyume na kanuni za soka. Yanga ilianza kipindi cha pili kwa kufanya mashambulizi mengi langoni mwa JKT Ruvu, lakini kipa Dihile na ngome yake walikuwa makini kuokoa hatari zote. Mshambuliaji Hamis Kiiza nusu aipate Yanga bao la kusawazisha baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa JKT na kupiga shuti lililotoa nje kidogo ya goli. Kocha wa JKT Ruvu, Charles Kilinda akizunguza baada ya pambano kumalizika aliwasifu wachezaji wake kwa kujituma na kufanikiwa kupata ushindi katika mchezo huo wa kwanza. Kwa upande wa Sam Timbe yeye alikataa kuzungumza na wanahabari kwa kisingizio cha kutaka chumba cha mkutano kitu ambacho hakipo kwenye uwanja wa Jamhuri. Vikosi Simba; Juma Kaseja, Amir Maftah, Juma Nyoso, Costa Victor, Jerry Santo, Patrick Mafisango, Salum Machaku, Felix Sunzu, Haruna Moshi, Emmanuel Okwi. Oljoro; Shahibu Issa, Omary Juma, Ally Hamza, Nurdin Seleman, Marcus Rafael, Ally Khan, Karage Musa, Sunday Paul, Roshuwa Rashid, Amir Hamad, Amoroso Seifu. Yanga: Said Mohamed, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua,Bakari Mbegu, Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Julius Mrope, Haruna Niyonzima, Pius Kisambale, Hamis Kiiza, Rashid Gumbo. JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Kessi Mapande, Stanley Nkomola, Shaibu Nayopa, Damas Makwaya, Geogre Minja, Amos Mgisa, Nashoni Naftari, Rajabu Chau, Hussen Bunu na Sostenes Manyasi.