Simba yatoa sababu kukwama mchakato uendeshaji klabu

KLABU ya Simba imekwama kukamilisha mchakato wa mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo baada ya serikali kuitaka  wafanye maboresho ya Katiba yao.

Hivi karibuni uongozi wa Simba ulitangaza Kamati ya maboresho ya Katiba hiyo ambayo ipo chini ya Mwenyekiti,  Hussein Kita ambaye leo Januari 18 ametangaza kukamilisha kupokea maoni ya wanachama juu ya maboresho hayo na kuyafanyia kazi.

Kita amesema kuwa baada ya kupitia maoni ya wanachama wao kamati ilikutana kujadili na kitengeneza rasimu ya Katiba na kuipeleka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambayo imepitishwa na kupelekwa kwa wanachama kuipitia kabla ya kujadiliwa na mkutano mkuu utakaofanyika keshokutwa Jumapili.

Alisema kuwa maelekezo ya maboresho hayo waliyapokea baada ya FCC kutoa maelekezo RITA na BMT ya kuwataka wayafanyie kazi ili mchakato wao wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ukamilike.

Kita aliyataja maeneo ambayo yalitakiwa kuboreshwa ni Mamlaka ya uteuzi wa Bodi ya Wadhamini, Nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ambayo kwa katiba ya sasa haisemi chochote, malengo ya simba yaelezwe wazi, namna ya kupata kolamu ya wanachama kwenye mkutano mkuu, chombo cha Simba Sports Holding Company Limited ambacho ndicho mmiliki wa hisa, asilimia 99 za hisa kumilikiwa na Bodi ya Wadhamini na asilimia moja kumilikiwa na mwenyekiti wa Bodo ya wadhamini.

"Tumekaa vikao vingi sana, lakini vikubwa vilikuwa vinne, awali tuliitwa na Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro kutuuliza kwanini mchakato wa uendeshaji wa klabu haukamiliki, tulimweza sababu zilizokuwa zinatukwamisha kila tunapofanya jitihada. Waziri alishirikisha wadau wote Simba, FCC, RITA, TFF na BMT.

"Lakini sasa hivi mchakato utakamilika mara tu wanachama watakapoitisha hii Rasimu ya Katiba kwenye mkutano mkuu, kwani BMT tumewapelekea na wametupa barua ya kuridhika na namna tulivyofanya kwa kufuata maelekezo yao, hivyo sasa ni jukumu la wanachama kuipitisha siku ya mkutano mkuu ingawa kikatiba tumewatumia kupitoa matawi ili waipitie na siku hiyo iwe kuijadili tu," alisema Kita.

Wakili Kita alisema maboresho hayo yatakuwa na faida kwa pande zote mbili klabu na wanachama kwani yatasaidia kukamilisja mfumo wao wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ambayo umekwama kwa zaidi ya miaka mitano.

Hivi sasa Simba ipo chini ya Bodi ya Wakurugenzi ambapo awali Mwenyekiti alikuwa ni Mohamed Dewji ambaye ni mwekezaji wa klabu hiyo lakini sasa bodi ipo chini ya Salim Abdallah 'Try Again' huku Murtaza Mangungu akiwa Mwenyekiti wa klabu akichaguliwa na wanachama.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Simba, Imani Kajula alisema kuwa; "Maboresho hayo yamechukuwa muda mrefu hadi hapo yalipofikia lakini Jumapili ndiyo itakuwa hitimisho kwa wanachama kuamua kuipitisha Rasimu hiyo. Hivyo mkutano mkuu ajenda kuwa itakuwa ni hiyo na kufautiwa na zingine,"