Simba yapindua meza kibabe, kibao chawageukia Yanga

Saturday October 10 2020
yanga simba pic

UKISIKIA kupindua meza ndiko huku. Si unakumbuka kabla ya kupanguliwa kwa pambano la watani lililokuwa lipigwe Oktoba 18, Simba walionekana watataabika mikoani kabla ya kuvaana na Yanga? Ratiba ya awali ilikuwa ikionyesha Simba ingecheza mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Tanzania kisha kuifuata Tanzania Prisons kabla ya kukutana na Yanga ambayo ilikuwa imepangwa kucheza mechi mbili mfululizo nyumbani. Kabla ngoma haijageuka.

Ratiba hiyo ya awali ilionyesha Yanga ingevaana na Coastal Union kisha Polisi Tanzania ndipo wacheze na Simba.

Hata hivyo, timu zote kila moja ilicheza mechi moja moja, Yanga kuigagadua Coastal Union kwa mabao 3-0 na Simba kuwanyoosha JKT ugenini kwa mabao 4-0 na zilizokuwa zikifuata wikiendi hii zikaahirishwa kupisha pambano la kirafiki la kimataifa la Taifa Stars dhidi ya Burundi.

Lakini wakati mashabiki wakianza tambo zao mtaani kwa ajili ya pambano hilo, ghafla Bodi ya Ligi (TPLB) ilitangaza kuahirishwa kwa mchezo huo hadi Novemba 7, kisha wakatoa ratiba mpya ambapo sasa kibao kimewageukia Yanga. Ndio, katika ratiba hiyo iliyotolewa jana na Bodi ya Ligi ni kwamba kabla ya pambano hilo la 105 kwa watani kukutana katika Ligi ya Bara tangu mwaka 1965, timu hizo zitakuwa na michezo minne.

Yanga na Simba kila moja itarejea uwanjani Oktoba 22 baada ya mapumziko mafupi ya ligi kwa kucheza mechi zao za viporo, Vijana wa Jangwani wataikaribisha Polisi Tanzania jijini Dar es Salaam huku wenzao wataifuata Tanzania Prisons mjini Sumbawanga.

Siku tatu baadaye, Yanga itakuwa safarini Kanda ya Ziwa kuwafuata KMC walioomba wakawavae Wanajangwani jijini Mwanza, Vijana wa Kinondoni wakiwa wenyeji, kisha Yanga watacheza dhidi ya Biashara United Oktoba 31 kisha kurejea Mwanza kucheza na Gwambina Novemba 3, ndipo irejee Dar es Salaam.

Advertisement

Mechi hizo zote kwa Yanga ni mtihani mzito kutokana na rekodi kuonyesha kwenye misimu miwili iliyopita, ikiwa mkoani Mara Yanga ilipasuka mara moja kwa kufungwa 1-0 kisha kujitutuma na kupata suluhu kwa msimu uliopita.

Wakati Yanga ikiteseka mkoani, Simba wao baada ya kumaliza kibarua chake kwa Prisons, itarejea Dar kwa kucheza mechi tatu mfululizo dhidi ya Ruvu Shooting itakayopigwa Oktoba 26 kabla ya kuialika Mwadui Oktoba 31 na kumalizana na Kagera Sugar Novemba 4 ndipo itavaana na Yanga wakiwa wageni kwa vijana hao wa Jangwani ambao msimu uliopita walivuna alama nne toka Msimbazi.

Kwa hesabu hizo na kwa rekodi ya Simba kwenye Uwanja wa nyumbani ni wazi itawakabili Yanga wakiwa na faida kubwa kama watazitumia mechi zao tatu za awali vizuri, tofauti na Yanga kwa mechi hizo tatu za ugenini kama watateleza wataikabili Simba kinyonge.

Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye alikataa kutajwa jina gazetini kwa madai kuwa kuna mambo mazito ya ndani ambayo bado wanajadiliana kuhusu ishu hiyo, alisema kuwa wataandika barua rasmi kwenda Bodi ya Ligi kuomba mchezo wao mmoja mkoani uahirishwe na wako kwenye hatua za mwisho.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto alipoulizwa kuhusu ratiba ya Yanga kufuatana mechi za ugenini huku wakiwa ni wenyeji katika pambano la watani wa jadi alisema: “Hilo suala la CEO, mpigie yeye atakupa majibu sahihi.”

Alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (CEO) Almas Kasongo alisema; “Siyo kila kitu kinachozungumzwa tukitolee ufafanuzi, hatuishi hivyo na hata hiyo mechi ya Prisons na Simba kuahirishwa mbona hata Yanga zao zimeahirishwa au Yanga hamjawaona?”

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominick Albinus alisema bado hawajaandika barua kuomba baadhi ya mechi zao ziahirishwe na anachofahamu ni kwamba watacheza mechi tatu kisha kuivaa Simba.

Kwa upande wa wadau, mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema; “Haya mambo hayatikiwi kuwa ya kujirudia mara kwa mara, lakini hapa ishakuwa katika hali ya kawaida lakini ukweli tunadumaza soka letu, hii inaweza kuleta shida.”

Mwalimu Kashasha ambaye ni mchambuzi alisema; “Kusafiri inategemea na umbali, mwalimu anatakiwa apate muda wa kurikava, pia kiufundi ratiba inapobadilika kwa ratiba mwalimu anapata tabu kubwa katika plani ya mechi husika lakini timu inabidi zikubali maana hamna namna.”

Advertisement