Simba yapewa mashabiki 60,000 dhidi ya Orlando

Muktasari:

  • Mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya USGN, idadi ya mashabiki walioruhusiwa walikuwa ni 35,000.

Wakati waamuzi wa mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba na Orlando Pirates, Jumapili Aprili 17 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakiwekwa hadharani, Simba imeruhusiwa kuingiza jumla ya mashabiki 60,000 katika mchezo huo.

Idadi hiyo ndio ukomo wa mwisho wa namba ya mashabiki ambao Uwanja wa Benjamin Mkapa inaweza kuingiza katika mechi moja.

Habari za uhakika kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na lile la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimefichua kuwa Simba imeruhusiwa kuingiza idadi hiyo ya mashabiki baada ya kupeleka ombi CAF.

"Simba wameruhusiwa kuingiza jumla ya mashabiki 60,000 Jumapili, Aprili 17 katika mechi yao dhidi ya Orlando Pirates," kilithibitisha chanzo chetu.

Idadi hiyo ya mashabiki imeruhusiwa ikiwa ni nyongeza ya mashabiki 25,000 kutoka ile ya mchezo uliopita baina ya Simba na USGN ambayo jumla ya mashabiki 35,000 ndio walioruhusiwa.

Hilo limekuja baada ya Caf kuweka hadharani majina ya waamuzi watakaochezesha mchezo huo.


Haythen Guirat kutoka Tunisia ndiye atakeyechezesha mechi hiyo akisaidiwa na Khalil Hassan (Tunisia), Samuel Pwadutakan (Nigeria) huku refa wa akiba akiwa ni Sadok Selmi wa Tunisia.


Mwamuzi wa VAR atakuwa ni Ahmed Elghandor atakayesaidiwa na Youssef Elbosaty wote wakiwa wanatoka Misri.


Ikumbukwe, refa Haythem Guirat ndiye alichezesha mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Simba na AS Vita iliyochezwa Aprili 3, 2021 ambayo Simba walipata ushindi wa mabao 4-1