Simba, Yanga zatiliwa ubani

Muktasari:

  • Simba inacheza leo na Horoya ya Guinea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kesho Yanga kuikaribisha Monastir ya Tunisia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na RC Homera alisema hizo mechi zitakazoipa heshima Tanzania

MBEYA. WAKATI Simba na Yanga zikitarajia kushuka uwanjani wikiendi hii kwenye mechi za kufa au kupona za michuano hya CAF zitakazopigwa jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amezitilia ubani akiziombea heri, huku akiwaomba wadau na mashabiki kuungana pamoja kuzisapoti.

Simba inacheza leo na Horoya ya Guinea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kesho Yanga kuikaribisha Monastir ya Tunisia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na RC Homera alisema hizo mechi zitakazoipa heshima Tanzania, hivyo bila kujali ushabiki lazima wadau na mashabiki wote waungane pamoja kuziombea na kuzisapoti ili zipate ushindi na kusonga mbele.

“Tunahitaji umoja na mshikamano kwenye hizi timu ili ziweze kushinda michezo hizo za leo na kesho, sisi kama watanzania lazima tuungane kwa maombi na kuzisapoti Simba na Yanga ili zifuzu robo fainali, hii ni heshima kwa taifa,” alisema Homera shabiki lialia wa Yanga.

Pia Homera hakusita kuzipongeza Ihefu na Mbeya City kwa kutinga  robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC)  na kuzitakia zifanye kweli mbele ya Simba na Singida Big Stars na kwenda nusu fainali ili kuzidi kuipa heshima Mkoa wa Mbeya na kubeba pia taji kwa mara ya kwanza.