Simba, Yanga zaivuruga JKU

PAMOJA na kupiga pesa kwa kuwauza mastaa wao, lakini JKU imejikuta katika kipindi kigumu kwa kusotea matokeo mazuri Ligi Kuu ya Zanzibar ‘ZPL’ na mashabiki kuhoji hatma ya timu hiyo kwenye mbio za ubingwa.
Timu hiyo kinara kwenye ligi hiyo kwa pointi 40, ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa taji msimu huu kutokana na walivyoanza kibabe mashindano hayo, lakini kwa sasa upepo umebadilika.
Katika mechi tatu za mzunguko wa pili, timu hiyo imeshinda mchezo mmoja dhidi ya New City bao 1-0, suluhu ya bila kufungana mbele ya Malindi FC na kupoteza dhidi ya Uhamiaji 1-0.
Maafande hao dirisha dogo iliwauza mastaa wao watatu waliokuwa tegemeo, ikiwa ni Shekhan Ibrahim aliyeenda Yanga, Saleh Karabaka (Simba) na Gamba Iddi Matiko aliyetua JKT Tanzania.
Mmoja wa mashabiki na mdau wa soka visiwani hapa, Abubakar Mwinyi alisema anashangazwa kuona timu hiyo imepata pesa nyingi ya mauzo ya wachezaji lakini imeshindwa kufanya usajili mzuri.
“Mimi nashangaa timu imeingiza hela kutoka Yanga, Simba na JKT Tanzania, inashindwa kununua wachezaji wengine wenye ubora ili kulinda matokeo yao, kwa hali hii naona ugumu wa ubingwa,” alisema Mwinyi.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Ali Haji alisema ni upepo mbaya tu ambao wanapitia kwa sasa, anaamini usajili walioufanya kuziba pengo la watangulizi wao watafanya vizuri.
“Huu ni upepo tu lakini naamini hata hawa walioingia kuziba pengo la wenzao watafanya vizuri ni suala la muda kwani benchi la ufundi linaendelea kuisuka timu kutengeneza muunganiko,” alisema Haji.
JKU wanakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Zimamoto Februali 23 kwenye uwanja wa Mao Zedong A, huku Maafande hao wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0.