Simba, Yanga yeyote anastahili Kombe la Mapinduzi

UNGUJA. Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanamalizika leo na watani wa jadi, Simba na Yanga watakutana kusaka bingwa. 
Simba na Yanga ndizo timu zilizocheza kwa kupambana zaidi kutaka matokeo mazuri na hii ilionyesha kila moja inahitaji ubingwa huo, hivyo atakayechukua anastahili kwani ni lazima uende kwa timu moja. 
Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye fainali za michuano hizo ilikuwa 2011, ambapo zilifanyika Uwanja wa Amaan mjini hapa. Mara nyingi kila moja kati ya timu hizo huishia nusu fainali au mwingine fainali, ambapo ni kama hukwepana. 
Katika mashindano ya mwaka huu ambayo yalipangwa makundi matatu, Yanga ilikuwa Kundi A pamoja na Jamhuri na Namungo, wakati Simba walikuwa kundi B na Chipukizi na Mtibwa Sugar. Azam FC ilikuwa Kundi C na Mlandege pamoja na Malindi ambazo kwa soka la Zanzibar ni kama Simba na Yanga kwa Bara. Malindi na Mlandege walitolewa baada kushindwa kufikisha pointi kama ilivyokuwa kwa Azam ambao walitinga nusu fainali. 
Azam FC iliongoza kundi lao ikiwa na pointi nne, Mlandege pointi mbili wakati Malindi ikimaliza na pointi moja. Kundi la Yanga wao ndio waliongoza wakiwa na pointi nne wakati Namungo walifuata kwa pointi tatu huku Jamhuri wakiambulia pointi moja. 
Simba waliibuka kidedea kwenye kundi kwa kukusanya pointi sita na mabao matano yaliyowapeleka nusu fainali wakati Mtibwa Sugar walishika nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu na bao moja, huku Chipukizi wakiaga mapema. 
Kwa namna ambavyo ratiba ilipangwa ilikuwa vigumu Simba na Yanga kukutana nusu fainali kutokana na makundi hayo. 
NUSU FAINALI 
Nusu fainali ilikuwa mshindi wa kwanza Kundi A waliokuwa Yanga walicheza na mshindi wa kwanza kundi C Azam FC. Yanga ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 lile la Yanga lilifungwa na Tuisila Kisinda wakati la Azam likifungwa na Obrey Chirwa. Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Meddie Kagere na Athuman Miraji ‘Sheva’. 
Mpaka sasa kabla ya fainali kupigwa Sheva ndiye kinara wa mabao akiwa amefunga manne, wakati Kagere ana mabao mawili. Huenda nyota hao leo wakaongeza mabao mengine au kubaki na hayo. 

Mtibwa, Azam FC mtihani mgumu
Mtibwa Sugar waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo waliondolewa hatua ya makundi baada ya kufungwa na Simba mabao 2-0 ingawa tayari walikuwa wameshinda mechi moja dhidi ya Chipukizi kwa bao 1-0. 
Kilichowaondoa Mtibwa kucheza nusu fainali kama ‘best looser’ ni uwiano wa mabao na Namungo ambao walishinda 2-0 katika mechi ya mwisho dhidi ya Malindi hivyo kuwazidi Mtibwa kwa bao moja. 
Upande wa Azam FC, wadau wengi walisikitika kutokana na kiwango cha chini walichocheza hasa mechi za makundi ukiachana na namna walivyocheza dhidi ya Yanga ambapo pia walifungwa kwa mikwaju ya penalti. 
Wachezaji wa Azam katika mechi mbili walicheza kana kwamba walifika kushiriki tu na sio kushindana hadi walipoamka wakati wanacheza na Yanga nusu fainali. 
Ni dhahiri kwamba ndani ya Azam kuna shida ingawa haijawa wazi na pengine hata viongozi hawajui matatizo yanayowafanya kupata matokeo mabovu kila uchwao. Mashabiki na wadau wengi waliikatia tamaa Azam kwani walitarajia vitu viwili kutoka kwao; matokeo mazuri na burudani ambavyo vyote walivikosa. 


Simba mabao, burudani
Pamoja na kwamba Simba iliwakosa baadhi ya nyota wao kama Clatous Chama na Luis Miquisson, lakini walicheza vizuri na kila hitaji kwa mashabiki wao walifanikiwa kulitoa. Walipata matokeo mazuri katika mechi zote na pia walitoa burudani kwa mashabiki wao. 
Simba pia ni miongoni mwa timu zilizotoa wachezaji wawili walioibuka wafungaji bora katika mechi mbili tofauti - Sheva na Francis Kahata. 
Mbali na hilo, ni timu ambayo wachezaji wake wanaongoza kwa mabao mengi ambapo Sheva anayo manne wakati Kagere mawili. Simba walistahili kuingia fainali kwani walionyesha nia tangu mwanzo mwa mashindano hayo ingawa walikuwa wametoka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wameingia hatua ya makundi. 


Wa kigeni Simba
Simba imekuja na wachezaji wa kigeni kwa ajili ya kufanya majaribio ambao ni Ian Nyoni, Kevin Moyo na Ategele Coulibally wote raia wa Zimbabwe, lakini hawajawashawishi hata mashabiki ambao wameonekana kutoridhishwa na viwango vyao. Simba hii ya kimataifa iliyotinga hatua ya makundi Afrika imeelezwa kwamba inapaswa kusajili wachezaji watakaoingia kikosi cha kwanza moja kwa moja na sio wa majaribio, lakini yote aachiwe kocha msaidizi Seleman Matola na mabosi namna watakavyoamua juu ya usajili wa wachezaji hao kama ambavyo Taddeo Lwanga anavyoendelea kukaa sawa kiafya. 


Sarpong maji kupwa, maji kujaa
Sarpong ndiye straika anayetegemewa Yanga, lakini kwenye mashindano ameonekana kucheza kwa kiwango cha chini hasa kushindwa kuwa na kasi akidondokà zaidi kuliko kumiliki mipira. 


Yanga wanajaza kuliko Simba
Mwanaspoti ambayo imepiga kambi visiwani hapa imeshuhudia mechi za mashindano haya zikiwa na uzito na ujazo tofauti wa mashabiki uwanjani. 
Mwanaspoti lilishuhudia mechi za Yanga hasa ilipocheza na Namungo uwanja ulifurika, lakini ni tofauti wakati Simba ikicheza na Mtibwa Sugar au Namungo ambapo hawakujaa kuizidi Yanga. Lakini katika mechi za nusu fainali mashabiki walijitokeza kwa wingi kwenye mechi zote mbili na hii ilichangia kwamba kila mtu alitaka kuona nani anaingia fainali. 
Hata hivyo, Unguja ina mashabiki wengi wanaoipenda Yanga kuliko Simba ambao mashabiki wao wengi wapo Pemba. 


BURUDANI 
Kamati ya mashindano pia iliandaa burudani kwa mashabiki zilizotolewa na Jux, Meja Kunta waliotumbuiza kwenye mechi za makundi na nusu fainali ambapo kwenye fainali wanatarajia kuwepo Harmonize na Nandy. 
TIMU ZA ZANZIBAR 
Zanzibar iliwakilishwa na timu nne - kutoka Pemba ilikuwa Chipukizi na Jamhuri ambazo zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza wakati Unguja kulikuwa na Malindi na Mlandege ingawa hazikuonyesha ushindani mkubwa. 
Baadhi ya makocha wa timu hizo walisema vijana wao walijitahidi kushindani ingawa isingekuwa rahisi kuziondoa timu za Bara. “Tumejifunza mengi kupitia mashindano haya lakini kubwa ni mbinu kutoka kwa wazoefu kama Simba, Yanga, Azam, Mtibwa na Namungo ambazo zitatusaidia kwenye ligi zetu,” anasema kocha wa Chipukizi, Mzee Ali Abdallah.

 
WAAMUZI NA POSHO 
Waamuzi ndio wenye uamuzi wa mwisho kwenye mechi, lakini wakati wa mashindano kulikuwa na malalamiko hawafuati sheria 17 za soka. 
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema: “Sio kwetu tu, bali hata timu zingine waamuzi hawatoi uamuzi sahihi, nimelipeleka kwa viongozi na waliahidi kulifanyia kazi.” 
Kwa kawaida timu hugharamiwa na waandaaji kwa kila kitu kuanzia usafiri, maradhi na chakula hivyo pesa inayopatikana kwenye mechi haigawiwi kwa timu. 
Hata hivyo posho za timu za Zanzibar ni tofauti na zile za Bara ambazo pia inadaiwa zimegawanyika. Timu za Zanzibar imeelezwa hupewa Sh3 milioni kwa siku zote ambazo huwapo kwenye mashindano wakati zile za Bara hupata zaidi ya Sh10 milioni. 


SIMBA YAONGOZA TUZO ZA MVP 
Katika mashindano hayo kila mechi ilikuwa na Mchezaji Bora ambapo hadi nusu fainali walipatikana MVP 11, Juma Nyangi (Mtibwa Sugar), Ali Juma Ali (Jamhuri), Jaffar Maneno na Hafidh Abeid (Mlandege), Kibwana Shomari (Yanga), Eric Kyaruzi (Namungo), Francis Kahata na Miraji Athuman (Simba), ambao walipatikana hatua ya makundi na kila mmoja alizawadiwa Sh 200,000 wakati wale waliopatika nusu fainali Haruna Niyonzima (Yanga) na Yassin Mzamiru (Simba) ambapo walipewa Sh 500,000 kila mmoja.