Simba, Yanga wazungumzia wagombea urais

Cannavaro na Busungu
Muktasari:
Mpaka sasa ni zaidi ya wagombea kumi wametangaza nia za kugombea nafasi hiyo nyeti ambapo baadhi yao ni Edward Lowassa, Samuel Sitta, Steven Wasira, Mwigulu Nchemba, Mark Mwandosya, Sospeter Muhongo, Fredrick Sumaye, Dk. Khamis Kigwangala, Makongoro Nyerere, Lazaro Nyarandu, William Ngeleja na Titus Kamani wakati Bernard Membe anatarajia kutangaza nia kesho Jumamosi. Wote hao ni makada wa chama tawala cha CCM.
WACHEZAJI mbalimbali wa soka wametoa maoni na mtazamo wao kuhusiana na wanachama wa vyama mbalimbali waliojitokeza na kutangaza nia kuwania urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa nchi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Mpaka sasa ni zaidi ya wagombea kumi wametangaza nia za kugombea nafasi hiyo nyeti ambapo baadhi yao ni Edward Lowassa, Samuel Sitta, Steven Wasira, Mwigulu Nchemba, Mark Mwandosya, Sospeter Muhongo, Fredrick Sumaye, Dk. Khamis Kigwangala, Makongoro Nyerere, Lazaro Nyarandu, William Ngeleja na Titus Kamani wakati Bernard Membe anatarajia kutangaza nia kesho Jumamosi. Wote hao ni makada wa chama tawala cha CCM.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ yeye anamuunga mkono Mwigulu na kuwaomba Watanzania kumuunga mkono mgombea huyo ili aweze kuleta maendeleo nchini hasa kwenye sekta ya michezo.
Cannavaro alisema: “Mwigulu ni mmoja wa viongozi makini niliopata kuwaona nchini, ni kijana na tumekuwa tukiona uzalendo wake kwa kuwa na tabia ya kupenda nchi.
“Sina shaka na elimu yake, sina shaka na utendaji kazi wake. Naamini akipewa nafasi anaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye nchi na ndani ya miaka mitano na umasikini utapungua.”
Straika mpya wa Yanga, Malimi Busungu alisema: “Mimi ninaangalia sera na utendaji wa kiongozi kabla hajapata. Mimi ninamtizama Membe kama mtu ambaye anaweza kuwa na faida kwa wananchi, naamini akifanikiwa kushinda itakuwa neema kwa Watanzania kwa kuwa ni mtu wa watu na mtu ambaye anapenda haki sawa kwa kila Mtanzania.
“Atatoa matabaka ya walichonacho na wasionacho na hapo tutaweza kutengeneza Tanzania mpya ambayo kila mtu atafanya kazi na kunufaika na kazi yake na hii inatokana na uchapaji kazi wake tuliokuwa tukiuona, lakini pia hajajihusisha kwenye kashfa yoyote ile. Pia kwa kipindi chote akiwa Waziri wa Mambo ya Nje naamini amekuwa moja ya watu waliochangia Tanzania kuwa na amani na kutengeneza mshikamano na mataifa mengine.”
Beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul alisema: “Nisingependa kuzungumza kwa niaba ya mtu yeyote, mimi binafsi nampa nafasi Mwigulu, ni mtu makini, anajua nini Tanzania inahitaji miaka inayokuja. Pia binafsi ninamuona kama kijana anayejua vijana wenzake wanapitia nini.”
Beki wa kushoto wa timu hiyo, Oscar Joshua alisema: “Tumekuwa na wakati mgumu kwenye nchi yetu. Wengi wetu ni masikini, hivyo muda huu ni muda wa kutafuta mabadiliko. Mheshimiwa Mwigulu anaweza kuwa mkombozi wetu kwenya hili janga la umasikini.
“Kama wachezaji wa soka tutaacha kulaumiwa na hiyo inatokana na mipango ya kuwekeza kwenye soka la vijana ambayo tumekuwa tukimsikia akilizungumzia.”
Kwa upande wa kipa wa Simba, Ivo Mapunda alisema: “Siwezi kusema nani anafaa kati ya wote waliotangaza nia zao ingawa nimebahatika kusikiliza hotuba zao kwa umakini mkubwa, kikubwa ambacho nakiona ni Kamati Kuu ya CCM kuchagua mtu watakayemsimamisha ambaye hana kashfa za ufisadi.
“Kwa asilimia kubwa wote waliotangaza nia wana kashfa za ufisadi, nchi yetu sasa inatakiwa iongozwe na rais ambaye ana sifa nzuri, ni msafi na hapo ndipo ninapoweza kusema ni rais gani anayeweza kutusaidia hata kwenye michezo, nimemsikiliza Profesa Muhongo kazungumzia michezo kwa asilimia ndogo sana wakati kwa nchi za wenzetu michezo ndiyo inayowaunganisha watu wa aina zote.”
Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema: “Rais Kikwete ni mpenda michezo ndio maana aliweza kubadilisha kwa kiasi fulani ila hawa wajao na kutangaza nia kwa kweli siwezi kuzungumzia lolote, tusubiri tuone na kuchagua tu atakayetufaa.Kufaa siyo kwenye michezo peke yake bali ni katika nyanja zote za maendeleo ya jamii nchini.”
Naye kiungo wa Simba, Jonas Mkude, alisema: “Mimi ninachosubiri ni kiongozi bora, yeyote atakayepitishwa naamini atakuwa na sifa. Kikubwa si jina, ila ni uwezo wa kufanya kazi.”