Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga, riadha kunogesha tamasha la Chato

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mwanza. MCHEZO kati ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga utakuwa miongoni mwa burudani zitakazopamba tamasha la Chato litakalofanyika kwa siku saba kuanzia Novemba 26 hadi Desemba 3, 2023 katika Uwanja wa Magufuli wilayani Chato Mkoa wa Geita, lenye lengo la kutangaza vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji na biashara na kukusanya fedha zitakazosaidia kununua madawati 29,000 katika shule mbalimbali wilayani humo.

Mchezo huo wa watani utapigwa Novemba 29, mwaka huu huku michezo mingine ikiwa ni mbio za baiskeli kilometa 80 (Chato –Katete), mashindano ya mitumbwi kilometa 8 (Kisiwa cha Rubondo –Mwerani), mapambano ya ngumi na riadha kilometa 5, kilometa 10 na kilometa 21 ambazo washiriki watajiandikisha kwa Sh30,000.

Hayo yameelezwa leo Novemba 16, 2023 na mmoja wa waratibu wa tamasha hilo, Ombeni Hingi ambaye ni mhifadhi Mwandamizi hifadhi ya taifa Burigi -Chato, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu maandalizi ya tamasha hilo lenye lengo la kuitangaza Chato kimataifa na kuifanya kuwa kitovu cha utalii.

“Mechi hii itaratibiwa na viongozi wa juu wa hizi timu mashabiki kutoka sehemu mbalimbali wataunda timu na kucheza ni mchezo wa furaha na burudani, tunategemea itakuwa fursa nzuri kwa viongozi wao kufurahia na mashabiki kwa sababu wasemaji Ali Kamwe na Ahmed Ally wameshiriki mwanzo wa mchakato huu na waliahidi kuwepo,”

“Tunatumia jukwaa hili kutangaza utalii na kuwakaribisha watanzania kutembelea vivutio vya utalii. Hifadhi ya Burigi Chato ni ya nne kwa ukubwa nchini ina maziwa matano ni hifadhi nzuri kuitembelea ina vivutio vyote muhimu tunategemea kwamba Watanzania wengi watafika na kuwa mabalozi wetu ili kuchangia ukuaji wa uchumi,” amesema Hingi

Naye, Afisa Mhifadhi Kisiwa cha Rubondo, Themistocles Mbita, amesema tamasha hilo litakuwa na mfululizo wa matukio ya burudani kwa siku saba ikiwemo safari za kutembelea hifadhi kila siku na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa muziki wa asili na kizazi kipya na kuifanya Chato inoge, huku akiwaomba Watanzania kushiriki kwa wingi tamasha hilo, kutembelea hifadhi, kujifunza fursa mbalimbali na kuchangia pato la taifa.

“Tamasha hili ni ndoto ya wana Chato kuifanya kuwa ya kimataifa, Chato iliyochangamka na iwe kitovu cha utalii pia tuifanye kuwa eneo ambalo lina maendeleo watu wanataka kuiona Chato inabadilika. Kisiwa cha Rubondo tuna utalii wa ziwani (kupanda boti), utalii wa uvuvi, sokwe, kutembea kwa miguu na kuangalia vivutio ukiwa ndani ya gari,”


“Kutakuwa na mfululizo wa matukio kuanzia Novemba 26 mpaka Desemba 3 ambayo ni pamoja na ufunguzi utakaopamba na mbio za baiskeli, itafuata semina ya biashara na uwekezaji, mbio za mitumbwi, mechi ya mashabiki wa Simba na Yanga, kliniki ya biashara, pambano la ngumi, riadha, mkesha wa nyama choma ndani ya kivuko na kufunga tamasha,” amesema Mbita

Mdau wa utalii Kanda ya Ziwa, Laurent Laurian, amesema Watanzania watakaoshiriki tamasha hilo watafanikiwa kutembelea hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo kwa Sh45,000 safari ya kutwa na Sh75,000 kulala hifadhini, huku watakaokwenda hifadhi ya Burigi –Chato wakilipa Sh100,000 ambapo gharama hizo ni kwa ajili ya kiingilio, chakula, utalii wa matembezi na vinywaji na safari hizo zitafanyika kwa siku zote saba za taamsha hilo.