Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga ni ng’adu kwa ng’adu

Watani Pict

Muktasari:

  • Timu hizo kongwe kwenye soka la Tanzania, zimekuwa zikibadilishana ubingwa wa ligi hiyo kwa muda mrefu tangu 1965 ambapo Yanga imebeba mara 30 ikiwaongoza wote ikifuatiwa na Simba (22), lakini ndani ya kipindi cha miaka 20 kuanzia 2005 hadi msimu uliopita 2023-2024, mataji 19 yamebebwa na timu hizo kwa maana ya Yanga (12) na Simba (7) huku msimu wa 2013–14 pekee Azam ikibeba hiyo mara moja.

HII ni vita ya watani wa jadi, yaani ng’adu kwa ng’adu mpaka kieleweke. Unaweza kusema hivyo kutokana na namna Simba na Yanga zinavyokabana koo pale juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara zikiwa zote zimemaliza duru la kwanza kwa kucheza mechi 15 kila moja ikisubiri awamu ya pili kumaliza msimu huu.

Timu hizo kongwe kwenye soka la Tanzania, zimekuwa zikibadilishana ubingwa wa ligi hiyo kwa muda mrefu tangu 1965 ambapo Yanga imebeba mara 30 ikiwaongoza wote ikifuatiwa na Simba (22), lakini ndani ya kipindi cha miaka 20 kuanzia 2005 hadi msimu uliopita 2023-2024, mataji 19 yamebebwa na timu hizo kwa maana ya Yanga (12) na Simba (7) huku msimu wa 2013–14 pekee Azam ikibeba hiyo mara moja.

Hatua hiyo inadhihirisha kwamba Simba na Yanga ndio wababe wa Ligi Kuu Bara na kinachoendelea kwa sasa ni mwendelezo wa ubabe wao.

Baada ya kumaliza duru la kwanza, macho yote kwao yapo duru la pili ambapo kila moja ina hesabu zake kuhakikisha mechi 15 zilizosalia inazicheza kwa umakini mkubwa ili kufikia malengo ya kubeba ubingwa.

Ikumbuwe kwamba, Yanga ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo wakichukua taji kwa misimu mitatu mfululizo baada ya kuizidi kete Simba ambayo kabla ya hapo ilichukua mara nne mfululizo.

WT 01

Katika hesabu zao za duru la pili, Yanga wanaonekana hivi sasa timu yao imeanza kuimarika baada ya hapo katikati kuvurugika kidogo hali iliyofanya benchi la ufundi kubadilishwa akiondolewa kocha mkuu, Miguel Gamondi na msaidizi wake, Moussa N’Daw akaletwa Sead Ramovic akisaidiana na Mustafa Kodro ambapo pia ameongezwa Abdihamid Moalin aliyetoka KMC akiwa kocha mkuu na sasa ni mkurugenzi wa ufundi pale Jangwani, lakini pia akiwa sehemu ya makocha wasaidizi kikosini hapo.

Mabadiliko hayo yameendelea kuipa faida Yanga ambayo katika mechi tano zilizopita za ligi tangu Ramovic aiongoze timu hiyo, ameshinda zote na kufunga mabao 18 ikiwa na wastani wa mabao 3.6 kila mechi, wakati awali katika mechi 10 za kwanza timu hiyo ilifunga mabao 14 kwa wastani wa 1.4 kwa mechi.

Ile falsafa yao yao Gusa, Achia, Twende Kwao inaonekana kufanya kazi ndani ya Yanga huku sifa nyingi zikienda kwa kocha wa viungo wa timu hiyo, Adnan Behlulovic ambaye anatajwa kuimarisha utimamu wa wachezaji wa timu hiyo hali inayomrahisishia kazi Ramovic mbinu zake kukubalika.

WT 02

Simba yenyewe inaendelea na Ubaya Ubwela wake kwani inapambana kupata ushindi kwa njia yoyote ile ikiwamo kuwalazimisha wapinzani kufanya makosa kwenye eneo lao la hatari na kusababisha penalti kwani hadi sasa ndiyo timu iliyofaidika na mikwaju hiyo mara nyingi ambazo ni sita. Itakuwaje duru la pili kwenye mechi 15 zinazotajwa kwamba ndiyo zenye ushindani mkubwa kwani hata makocha wanalitambua hilo kutokana na kila mmoja kutumia muda huo kuweka hesabu zake sawa.


Mbio za ubingwa

Ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa sasa, Simba ndio vinara wakiwa na pointi 40, wakifuatiwa na Yanga (39), kisha Azam (36) na Singida Black Stars (33). Hizo ni nne bora ambapo Simba na Yanga kila moja imecheza mechi 15, Azam na Singida Black Stars zina mechi 16 ikiwa na maana kuwa zenyewe tayari zimeanza duru la pili.

Katika mbio za ubingwa unaoshikiliwa na Yanga, Simba katika mechi 15 imeshinda 13 sawa na Yanga, lakini ina sare moja iliyoipata kwa Coastal Union (2-2) wakati wapinzani wao hawana sare. Simba imepoteza mechi moja dhidi ya Yanga ilipofungwa 1-0 huku Yanga ikipoteza mbili mbele ya Azam (1-0) na Tabora United (3-1).

WT 03


Mabao

Katika ufungaji, hivi sasa Yanga inaongoza ikiwa na mabao 32 yaliyofungwa na wachezaji kumi tofauti yakiwamo mawili ya wapinzani kujifunga. Kinara wao wa ufungaji ni Clement Mzize mwenye sita, akizidiwa mawili pekee na kinara wa jumla, Elvis Rupia wa Singida Black Stars (8).

Katika mabao 32 ya Yanga, washambuliaji ni wanne waliofunga Mzize (6), Prince Dube (5), Kennedy Musonda (2) na Jean Baleke (1). Kwa upande wa viungo ni watano Pacome (5), Maxi Mpia Nzengeli (3), Stephane Aziz KI (2), Clatous Chama (1) Mudathir Yahya (1) na beki ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ (4). Mawili kutoka kwa wapinzani kujifunga ni Kelvin Kijiri (Simba) na Jackson Shiga (Fountain Gate). Mabao hayo ya Yanga, kipindi cha kwanza yamepatikana 17, wakati kipindi cha pili yakifungwa 15 ikionyesha nguvu yao kubwa ipo kipindi cha kwanza. Hata hivyo, mabao mawili pekee ndiyo ya penalti yote yakifungwa na Aziz Ki ambapo katika penalti tatu za Yanga msimu huu, moja wamekosa ikipigwa pia na Aziz Ki.

WT 04

Wakati Yanga ikiwa hivyo, upande wa Simba yenye mabao 31, hakuna ambalo wapinzani wamejifunga, huku yote yakifungwa na nyota wao 11 tofauti zikiwamo penalti sita, tatu zikifungwa na Leonel Ateba na nyingine Jean Charles Ahoua, hakuna mkwaju ambao Simba imekosa.

Kinara wa mabao Simba ni kiungo Jean Charles Ahoua mwenye saba. Ukiachana na Ahoua, viungo wengine wa Simba waliofunga ni Fabrice Ngoma (3), Edwin Balua (2), Awesu Awesu (2) na Debora Mavambo (1). Mabeki wamefunga Che Malone Fondoh (2), Shomari Kapombe (2) na nahodha Mohamed Hussein (1) wakati washambuliaji ni Leonel Ateba (5), Steven Mukwala (4) na Valentino Mashaka (2).

  

WT 05

Ulinzi

Safu ya ulinzi ya Simba imeonekana kuwa imara zaidi ikiongozwa na kipa Moussa Camara mwenye clean sheet 12 katika mechi 15 alizodaka huku akiruhusu mabao matano pekee ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi ikifuatiwa na Yanga (6) huku kipa wake namba moja, Djigui Diarra ambaye kwa sasa ni majeruhi akiwa na clean sheet saba. Kwa ujumla Yanga katika mechi 15, imetoka uwanjani mara 12 bila ya kuruhusu bao kufuatia clean sheet saba za Diarra, Aboutwalib Mshery (3) na Khomeiny Abubakar (2). Nyuma yao, Azam imeruhusu mabao manane ikiwa na clean sheet 10 kutoka kwa Mohamed Musatafa (6) na Zuber Foba (4).


5 zijazo

Hivi sasa ligi imesimama hadi Januari 20, 2025 itakapoendelea lakini ratiba inaonyesha Simba mechi tano zijazo ni dhidi ya Tabora United (ugenini), Fountain Gate (ugenini), Tanzania Prisons (nyumbani), Dodoma Jiji (nyumbani) na Namungo (ugenini) kabla ya mechi ya sita kukabiliana na Azam.

Yanga mechi tano zijazo kwa mujibu wa ratiba ni dhidi ya Kagera Sugar (nyumbani), KenGold (nyumbani), JKT Tanzania (ugenini), KMC (ugenini) na Singida Black Stars (nyumbani).

Kama hakutakuwa na mabadiliko ya ratiba, basi tutashuhudia wakongwe hao wakikutana Aprili 13, 2025 ambapo Yanga itakuwa mwenyeji baada ya ile ya kwanza kushinda 1-0.


WT 06

Makocha wanasemaje?

Kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema: “Tunajivunia sana na rekodi yetu ya duru la kwanza, lakini tunajua kuwa safari bado ni ndefu. Hii ni hatua moja tu ya kufikia malengo yetu makubwa kwa msimu huu. Ufanisi huu haukuja kirahisi, kila mchezaji amejiweka tayari, ameweka juhudi nyingi, na ni matunda ya kazi ngumu ya kila mmoja wetu. Lakini tunatambua kuwa Ligi Kuu ina ushindani mkubwa na lazima tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili tuendelee kuwa bora zaidi.

“Tunataka kuhakikisha tunakuwa kama timu. Hatufai kujiingiza kwenye furaha ya sasa pekee, bali lazima tuendelee kujitolea zaidi ili tuwe bora. Tunasonga mbele kwa kasi na tunatarajia kufanya vizuri zaidi.”

Naye Sead Ramovic wa Yanga amesema: “Tunataka kucheza soka la kasi kubwa, hili linahitaji wachezaji kuwa tayari kila wakati. Hatufai kumwacha mpinzani apumue, lazima tuwepo kwao kila wakati. Tunahitaji muda, bado hatujafika katika kiwango kinachohitajika, lakini tumepiga hatua nzuri. Tuko kwenye njia sahihi, Alhamdulillah. Tunashukuru kwa mafanikio haya na tunajivunia kwamba timu inaendelea kuimarika.”