Simba, Yanga nani zaidi?

MIAMBA ya soka la Tanzania Simba na Yanga, imeingia makubaliano na Azam Media, Azam Pay na Agrinfo kwa kuendesha shindano la 'Nani zaidi' kwa wanachama na mashabiki wa timu hizo mbili kubwa nchini.
Nani zaidi ni shindano la wanachama wa Simba na Yanga kupiga kuru kwa timu zao ambazo kura moja itakuwa gharama ya Sh1000 na zile pesa zitakazo patikana zitapelekwa kwa timu hizo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema hilo jambo ni la pili kwao kwani walianza kulifanya hapo awali ila kwa njia nyingine na walishindwa kwenda nalo hadi mwisho kutokana na ugumu wa ratiba waliyokuwa nayo.
Barbara amesema wakati wa awamu ya kwanza jambo hilo lilikuwa na changamoto wa ratiba kwangu walikuwa na mechi ngumu za Ligi Kuu Bara mfululizo pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika.
Amesema pesa zao ambazo watazipata katika mchakato huo watapeleka kwenye ujenzi wao wa uwanja Mo Bunju Arena kama ilivyokuwa katika awamu ya kwanza ya mchakato wao.
“Kwenye mambo muhimu ya kiuchumi kama hili shindano la Nani zaidi, Simba na Yanga tunatakiwa kushikamana na kuwa kitu kimoja ili kufanikisha na kila kitu kwenda vizuri bila ya kujali usjindani wetu wa dakika 90,” amesema na kuongeza;
“Pesa zetu zote zitakazokuwa zinapatikana tutaweka kwenye ujenzi wa uwanja, kwani tayari tumeshafahamu gharama yote, tumepima na tunayo michoro tayari ya aina ya uwanja tunao hitaji,”
“Nilienda Doha kuangalia baadhi ya viwanja, gharama na utengenezaji wake kama ambavyo alifanya Mwenyekiti wetu, Murtaza Mangungu aliyeenda Uturuki kufanya jambo kama hilo na nambk yalikuwa mazuri kwahiyo pesa hii tunaenda kuiweka uwanjani yote.”
Meneja wa habari wa Simba, Ahmed Ally amesema ushindani wao wanauacha uwanjani na linapofika suala la kiuchumi kama hilo Simba na Yanga wanakuwa kitu kimoja ili kulikamilisha na kwenda vizuri.
Ally amesema kwa mwaka Simba inalipa zaidi ya Sh200 milioni kwa ajili ya kulipa gharama ya kambi kwahiyo wakipata pesa hizo na kujenga uwanja watakuwa wamepunguza gharama kubwa.
Amesema pesa hizo ambazo mashabiki wa Simba watachanga wataenda kutengeneza miundombinu ya uwanja wao ili kukamilisha mchakato wa ujenzi kwani watakuwa wameokoa pesa nyingi wanazotumia wakati huu.
“Hili ni jambo la maendeleo Simba na Yanga tunatakiwa kuwa kitu kimoja ili kulikamilisha na kufanikiwa na naimani itakuwa hivyo,” amesema Ally.
Kwa upande wa Yanga, Ofisa mtendaji mkuu, Senzo Mazingisa amesema hilo ni jambo kubwa hata klabu mbalimbali zimekuwa zikitumia kwenye maendeleo ya timu.
“Tumeungana Simba na Yanga kusimamia hili jambo na naimani mashabiki wetu wataacha kubishana kwenye maeneo mbalimbali na wataamia huku ili kufanikisha klabu inakuwa washindi na kupata pesa za maemdeleo,” amesema Senzo.
Msemaji wa Yanga, Haji Manara amesema pesa zao hawatapeleka katika ujenzi wa uwanja kama ilivyo kwa wapinzani wao Simba bali watakwenda kuzifanyia kazi kwenye mambo muhimu.
“Suala la kujenga uwanja kwetu Yanga kuna mpango wake mwingine kabisa si pesa hizi ambazo wanachama na mashabiki wetu naimani watachanga na kuwa nyingi kuliko wapinzani, amesema Manara.
“Nitaenda kuhamasisha vya kutosha ili kuona Yanga inakuwa vinara kwa kuchangiwa pesa nyingi katika shindano hili na Nani zaidi.”