Simba yamuomba Mghana Azam

Muktasari:

  • Simba inahitaji kushinda mechi zote sita zilizosalia kwenye Ligi Kuu Bara ili kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 lakini sasa imeweka matumaini yao katika mechi kati ya wapinzani wao Yanga na Azam ambapo kama mambo yatakwenda sawa watakuwa na uhakika wa kuondoka na taji hilo.

APRILI Mosi ni siku ya Wajinga Duniani. Yanga na Azam zitacheza siku hiyo kwenye Uwanja wa Taifa. Straika wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ hatakuwepo kwenye mchezo huo kwavile ni majeruhi lakini Simba, wamemuomba Mghana Yahya Mohammed awaokoe kwa kuituliza Yanga.

Simba inahitaji kushinda mechi zote sita zilizosalia kwenye Ligi Kuu Bara ili kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 lakini sasa imeweka matumaini yao katika mechi kati ya wapinzani wao Yanga na Azam ambapo kama mambo yatakwenda sawa watakuwa na uhakika wa kuondoka na taji hilo.

Simba inasafiri kwenda Kanda ya Ziwa mwishoni mwa mwezi huu ambapo mapema mwezi ujao itacheza mechi tatu dhidi ya Kagera Sugar, Toto Africans na Mbao FC. Wakati Simba ikiondoka jijini Dar es Salaam kutakuwa na mchezo kati ya Yanga na Azam ambao ndiyo umeshika hatma yao.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema wanaomba Yanga ifungwe katika mchezo huo ili wao wawe  na akiba kubwa ya pointi ambapo watahitaji kushinda mechi tano tu ili kuweza kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu.

“Tunazitazama kwa mapana mechi za Kanda ya Ziwa, tunafahamu wazi kwamba kama tutaweza kushinda zote tutakuwa katika nafasi nzuri ya kushinda ubingwa,” alisema Manyanja ambaye amewahi kuzinoa Kagera Sugar na Coastal Union.

“Tunaitazama mechi ya Yanga na Azam, kama Yanga itapoteza mchezo huo ama wakatoka sare itakuwa nafuu kubwa kwetu, tutaweza kupata ubingwa mapema zaidi,” alieleza kocha huyo anayesubiri mbeleko ya Yahya Mohammed.

Mayanja alidai kwamba kwa sasa mipango yao inakwenda vizuri na leo Alhamisi wataanza mazoezi rasmi kujiandaa na michezo hiyo migumu wakifahamu wazi kwamba wanakwenda kukutana na timu zenye ushindani mkubwa. “Tutaanza mazoezi kesho (leo) ili tuweze kujiweka sawa kwa mechi hizo. Tufahamu kwamba zitakuwa ni mechi zenye ushindani mkubwa,” alisema.

STAND WAMHURUMIA PASTORY

Uongozi wa Stand United umeshtushwa na kushuka kwa kiwango cha straika wao wa zamani Pastory Athanas ambaye kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha Simba.

Katibu Mkuu wa Stand United, Kenny Nyangi alisema “Hatuwezi kujua kwanini ameshuka lakini huenda Stand tulimwamini na akapewa mechi nyingi maana alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha kwanza. Ni tofauti na sasa ambapo anaonekana anacheza dakika chache ingawa undani wa mambo hayo anayajua yeye na mabosi zake.”

Kwa upande wa maneja wake, Muhibu Kanu alisema changamoto inayomkabili mteja wake ni kukosa nafasi mbele ya mastraika wenye uzoefu kama Ibrahim Ajibu na Laudit Mavugo.

“Kikubwa namshauri awe mvumilivu na anapopewa nafasi ajaribu kuiheshimu akijua kuna wachezaji nyuma yake wanaimendea, naamini baada ya muda atafanikiwa kwa kuwa ana umri wa miaka 23 bado ana nguvu ya kupambana kutimiza ndoto zake” alisema. Simba wanaamini baadaye atarudi kwenye fomu yake.